MWANACHAMA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Simon Msigwa, ameikosoa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kufuatia taasisi hiyo kukabidhi gawio la shilingi bilioni 38.8 kwa Serikali, akisema mafanikio hayo hayana maana ikiwa wananchi wengi bado hawajapatiwa Vitambulisho vya Taifa licha ya kujiandikisha kwa miaka mingi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wa X, Msigwa amesema alijiandikisha kupata Kitambulisho cha Taifa mwaka 2017 akiwa Iringa Mjini, lakini hadi sasa hajakipokea.
Ameeleza kuwa hali hiyo si ya kwake pekee, bali inawakumba pia maelfu ya Watanzania wanaoendelea kusubiri huduma hiyo muhimu.
Msigwa amesema hakuna taasisi inayopaswa kupongezwa kwa kupeleka fedha Hazina wakati huduma yake ya msingi bado inakabiliwa na changamoto zinazowaathiri wananchi.
Kwa mujibu wake, gawio haliwezi kuwa kipimo cha mafanikio ikiwa wananchi wanaendelea kubeba gharama za ucheleweshaji na mfumo usiofanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, amesisitiza kuwa jukumu kuu la NIDA ni kuhakikisha kila Mtanzania anayestahili anapata Kitambulisho cha Taifa kwa wakati, huku akihoji sababu zinazoifanya taasisi hiyo ishindwe kumaliza changamoto ya ucheleweshaji wa utoaji wa vitambulisho wakati ikitangaza mafanikio ya kifedha.
Katika hoja zake, Msigwa amehoji chanzo cha mapato yaliyowezesha kutolewa kwa gawio hilo, kiwango cha fedha kilichowekezwa kuboresha uchapishaji na usambazaji wa Vitambulisho vya Taifa, pamoja na sababu zinazosababisha baadhi ya wananchi kusubiri huduma hiyo kwa miaka mingi baada ya kujiandikisha.
Amehitimisha kwa kusema kuwa mafanikio ya taasisi za umma hayapaswi kupimwa kwa kiwango cha fedha zinazokabidhi Hazina pekee, bali kwa ubora wa huduma zinazowafikia wananchi, akieleza kuwa mafanikio ya kweli ya NIDA yataonekana pale ambapo kila Mtanzania aliyesajiliwa atapatiwa Kitambulisho chake bila ucheleweshaji.