JAJI Mstaafu Joseph Sinde Warioba amesema haoni uwezekano wa Tanzania kukamilisha mchakato wa kupata Katiba mpya na kuwa na Katiba hiyo ifikapo mwaka 2029.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Warioba amesema hayo leo 28 Agosti 2026, wakati akizungumza katika Jukwaa la Demokrasia, akisisitiza kuwa Serikali inapaswa kutafuta njia mbadala za kushughulikia changamoto zilizopo nchini.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kuendelea na uchaguzi bila kwanza kushughulikia hoja na changamoto zinazoikabili nchi kunaweza kulisababishia taifa madhara makubwa.
“Kuhusu kupata Katiba nilisema mimi sioni uwezekano wa kupata Katiba kufika mwaka 2029, sioni uwezekano wa hiyo,” amesema Warioba.
Aidha, Jaji Warioba amesema wananchi bado wanaendelea kuomboleza kutokana na yaliyotokea Oktoba 29, 2025, akieleza kuwa hali hiyo haiwezi kupuuzwa.“Bado tunaomboleza. Wananchi wanaomboleza, lakini ukiangalia kama Serikali naona hakuna kikubwa,” amesema.
Amesema madhara na majeraha yaliyotokea ni makubwa na kwamba si jambo la busara kwa taifa kuendelea kana kwamba yaliyotokea yatasahaulika na maisha kurejea katika hali ya kawaida.
“Madhara tuliyopata, majeraha tuliyopata ni makubwa na inaonekana ni kama tunakwenda kwa mwenendo wa kusema, twende hivi, yatasahaulika, tutaendelea kama kawaida,” amesema Jaji Warioba.
Ameonya kuwa ni muhimu changamoto hizo kushughulikiwa kwa umakini ili kuweka msingi wa utulivu na mustakabali mzuri wa taifa.