ALIYEKUWA mbunge wa Iringa Mjini,Peter Msigwa amesema kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, hastahili kuwa gerezani kwa kuwa uwezo wake wa kiakili ni rasilimali muhimu inayopaswa kutumika katika maendeleo ya taifa.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza katika kipindi cha Medani za Siasa kinachoendeshwa na Chief Odemba, Msigwa alisema kuwa hata alipokuwa ndani ya CCM aliwahi kueleza kuwa Lissu si mhaini na kwamba kuendelea kumuweka mahabusu hakusaidii chama tawala wala taifa.
“Nilisema Lissu si mhaini tangu nikiwa CCM. Kumuweka ndani Lissu CCM haiwasaidii, ni kumuonea na kudhulumu maisha yake,” alisema Msigwa.
Aidha, Msigwa alieleza kuwa aliwahi kushauri kuwa Lissu ndiye anayefaa kuiongoza Chadema akisisitiza kuwa mawazo na uwezo wake wa kisiasa vinapaswa kutumika kwa manufaa ya nchi badala ya kuzuiwa.
“Akili ya Lissu haitakiwi kukaa gerezani. Ile akili inatakiwa itumike kuendeleza nchi, ni hazina. Kiongozi anayekimbia kuzungukwa na watu wenye akili hafai. Kiongozi mwenye busara hukusanya watu wenye uwezo wa kufikiri ili taifa lisonge mbele,” alisema Msigwa
Msigwa pia alisisitiza umuhimu wa kusikiliza mawazo ya upinzani, akieleza kuwa hoja na mapendekezo ya vyama vya upinzani yanapaswa kujadiliwa mezani kwa maslahi ya maendeleo ya taifa.