Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar
KILA Mtanzania sasa anadaiwa Sh. 1.8 milioni kutokana na deni la Taifa kufikia Sh.114.34 trilioni hadi kufikia Machi, 2026 kutoka Sh.107 Machi 2025. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Licha ya Serikali kutoweka takwimu za mgawanyo deni hilo kwa kila Mtanzaia, MwanaHALISI Online, limefanya mgawanyo wa deni hilo na kubaini kuwa kila Mtanzania anadaiwa takribani Sh. 1.8 milioni, kwa kuzingatia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, zilizonyesha idadi ya Watanzania ni milioni 61,741,120.
Akiwasilisha bungeni leo, tarehe 11 Juni 2026, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema deni hilo limetokana na mikopo iliyoelekezwa katika maeneo ya kimkakati yanayochochea ukuaji wa uchumi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, nishati na mawasiliano.
“Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanywa Novemba 2025 imeonesha kuwa deni ni himilivu katika kipindi cha muda wa kati na mrefu. Thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 39.6 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 55; deni la
nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 24.4 dhidi ya 15 ukomo wa asilimia 40; na deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.1 dhidi ya ukomo wa asilimia 180.” amesema.
Kwa mujibu wa Balozi Khamis, takwimu hizo zinaonesha kuwa Tanzania ina uwezo mzuri wa kusimamia na kuhimili deni lake bila kuathiri uthabiti wa misingi ya uchumi.