Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar
SERIKALI imesema itachukua hatua zaidi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuimarisha taasisi za ukusanyaji ili kukabiliana na kushuka kwa misaada na ufadhili kutoka nje. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo, tarehe 11 Juni 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27 ambapo amesema misaada kutoka nje imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka, hali inayofanya isiwe chanzo cha kuaminika cha mapato katika utekelezaji wa bajeti za taifa.
Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali itaongeza kasi ya kujitegemea kiuchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Kwa mujibu wa Balozi Khamis, utekelezaji wa miradi kwa fedha za mikopo umeendelea kukabiliwa na changamoto zinazohusiana na uhimilivu wa deni, gharama za mikopo pamoja na athari kwa uhuru wa kiuchumi wa nchi.
Amesisitiza kuwa hatua hizo zinalenga kuhakikisha taifa linakuwa na vyanzo imara vya mapato kwa ajili ya kugharamia maendeleo bila kutegemea kwa kiwango kikubwa misaada na mikopo kutoka nje.