MAKAMU Mwenyekiti wa Bara wa ACT Wazalendo na Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho, Isihaka Mchinjita, amemtaka Rais Samia kumwondoa madarakani Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, akidai ameshindwa kuwajibika katika masuala yanayohusu uhai na usalama wa raia.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Mchinjita alisema tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo, Mwigulu ameonyesha mwenendo unaoashiria ukosefu wa uwajibikaji, hususan kuhusu matukio ya mauaji ya wananchi yaliyotokea Oktoba 29, 2025 pamoja na madai ya kuendelea kwa vitendo vya utekaji nchini.
Alidai kuwa Waziri Mkuu ameonyesha msimamo huo kupitia kauli mbalimbali alizowahi kuzitoa katika ziara zake mikoani, mikutano na vyombo vya habari pamoja na mijadala ya Bungeni.
Mchinjita alirejea tukio lililotokea 30 Mei 2026 wilayani Manyoni, ambapo mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Abel alitoa ushuhuda mbele ya Waziri Mkuu akieleza kuwa mwanawe mwenye umri wa miaka 32 alichukuliwa nyumbani usiku na watu waliodaiwa kujitambulisha kama maafisa wa usalama.
Kwa mujibu wa maelezo ya mama huyo, watu hao walifika nyumbani kwake wakijionyesha kama wafanyabiashara wa mashuka kabla ya kujitambulisha kuwa maaskari na kumchukua mwanawe bila kutoa maelezo kuhusu kosa lolote. Alisema mwanawe alifungwa pingu na kuondolewa kwa nguvu mbele ya familia yake.
Mama huyo alidai kuwa jitihada zake za kufuatilia mahali alipo mwanawe hazijazaa matunda, ikiwemo kufika Kituo cha Polisi Manyoni mara kadhaa bila kupata taarifa zozote kuhusu alipopelekwa ambapo amesema zaidi ya siku 40 zimepita tangu tukio hilo litokee 21 Aprili 2026, na familia bado haijui hatima yake.
Mchinjita alisema tukio hilo ni mfano wa maumivu wanayopitia wazazi na ndugu wa watu wanaodaiwa kutoweka, kutekwa au kuuawa katika mazingira yasiyoeleweka nchini.
Aidha, aliishutumu serikali kwa kile alichodai kuwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya watendaji wa vyombo vya dola wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo hivyo, huku akitaka uwajibikaji wa viongozi wa juu wa serikali ili kurejesha imani ya wananchi katika taasisi za dola.