MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu, leo Jumanne 2 Juni 2026 amefikishwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kusikilizwa kwa maombi aliyowasilisha ya kutaka kuunganishwa katika kesi iliyokuwa ikihusu mgawanyo wa rasilimali za chama hicho kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kesi hiyo ya msingi ilikuwa imefunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamedi, pamoja na wenzake wawili dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Chadema kupitia Katibu Mkuu wake.
Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo 28 Mei 2026 kwa maelezo kwamba walalamikaji hawakuonyesha ni wakati gani hasa malalamiko yao yalianza.
Akizungumza mbele ya Jaji Ngunyale leo, Lissu alisema anaondoa rasmi maombi yake ya kuunganishwa katika shauri hilo kwa kuwa hayana tena msingi wa kisheria kufuatia kufutwa kwa kesi kuu aliyokuwa akitaka kujiunga nayo.
Hatua hiyo inaashiria kumalizika kwa maombi ya Lissu, baada ya kesi ya msingi ambayo yalikuwa yanategemea kutokuwepo tena mahakamani.