MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu Dodoma, imepanga kutoa uamuzi mnamo tarehe 23 Juni 2026 kuhusu maombi ya Tanganyika Law Society (TLS) ya kuunganishwa katika Shauri la Kikatiba Na. 7300 la Mwaka 2026 lililofunguliwa na Mawakili Kulwa William Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Mkuu wa Magereza na Mkuu wa Gereza la Ukonga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Maombi hayo ya TLS, Na. 12404 ya Mwaka 2026, yanasikilizwa mbele ya Mhe. Jaji Mruma kwa njia ya maandishi, ambapo pande husika zimeelekezwa leo Juni 02 kuwasilisha hoja na mawasilisho kwanjia ya maandishi kuanzia tarehe 8 Juni hadi 18 Juni 2026. Mahakama itatoa uamuzi wake kwa njia ya mtandao tarehe 23 Juni 2026 kuhusu iwapo TLS itaruhusiwa kuunganishwa katika shauri hilo au la.
Shauri hilo limetajwa leo Juni 02 ambapo TLS iliwakilishwa na Wakili Jebra Kambole, huku Mawakili Maduhu, Nashon na Kisabo wakitetewa na Wakili Mwandamizi Mpale Mpoki, John Seka, Ferdinand Makore na Edison Kilatu.
Shauri kuu la kikatiba Na. 7300 la Mwaka 2026 lilifunguliwa tarehe 23 Machi 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Kuu Dodoma. Shauri hilo lina hoja lukuki za kikatiba kupinga uhalali wa vitendo na vikwazo vya Jeshi la Magereza dhidi ya mawakili wanapofika gerezani kwa ajili ya kufanya mashauriano ya kisheria na mteja wao, Tundu Lissu.
Katika shauri hilo, Tundu Lissu ni sehemu ya wajibu maombi, na kupitia nyaraka zake za majibu ameainisha changamoto na vikwazo mbalimbali ambavyo yeye, mawakili wake, ndugu pamoja na wanachama wamekuwa wakikumbana navyo wakimtembelea gerezani.
Baada ya kufunguliwa kwa shauri hilo, Tanganyika Law Society ilionesha nia ya kujiunga katika kesi hiyo kutokana na masuala yanayoibuliwa kugusa moja kwa moja wajibu wa kitaaluma wa mawakili, haki ya kupata uwakilishi wa kisheria, pamoja na maslahi mapana ya utawala wa sheria nchini. Tarehe 19 Mei 2026 TLS iliwasilisha rasmi maombi ya kuunganishwa katika shauri hilo.
Aidha, shauri kuu la kikatiba limepangwa kusikilizwa tarehe 1 Julai 2026 mbele ya jopo la Majaji watatu ambao ni Mhe. Jaji Mruma, Mhe. Jaji Dkt. Rumisha na Mhe. Jaji Dkt. Longopa. Shauri hilo ni miongoni mwa mashauri muhimu yanayoweza kutoa mwelekeo kuhusu haki za mawakili kufanya mashauriano ya faragha na wateja wao waliopo mahabusu au magerezani.