WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amesema kuwa takwimu zinaonesha kupungua kwa matukio ya ukatili wa kingono nchini, ingawa wanawake bado wanaendelea kuwa waathirika wakuu wa vitendo hivyo. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
‎Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo 1 Juni 2026, bungeni jijini Dodoma, Dk. Gwajima amesema kuwa juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na serikali pamoja na wadau zimeanza kuzaa matunda katika kupunguza vitendo vya ukatili wa kingono.‎
‎Amesema takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa matukio ya ukatili wa kingono kwa jinsia zote yamepungua kutoka matukio 12,749 mwaka 2024 hadi matukio 11,625 mwaka 2025.
‎Hata hivyo, Waziri huyo amebainisha kuwa wanawake ndio wanaoathirika zaidi na ukatili wa kingono ikilinganishwa na wanaume.
‎Amefafanua kuwa wanawake 10,976 walikatiliwa kingono mwaka 2024 na idadi hiyo kushuka hadi 10,057 mwaka 2025. Kwa upande wa wanaume, waathirika walikuwa 1,773 mwaka 2024 na kupungua hadi 1,568 mwaka 2025.