KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ameitaka Serikali kuweka ruzuku kwenye bei ya mafuta pamoja na kuondoa baadhi ya tozo ili kupunguza gharama za maisha kwa Wananchi. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza leo tarehe 1 Juni 2026 katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema Jijini Dar es salaam, Mnyika amesema kushuka kwa bei ya mafuta katika Soko la Dunia kunatoa fursa kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza bei ndani ya Nchi.
Amesema Chadema inasisitiza Serikali ichukue hatua mbili kuu kupunguza tozo na kodi mbalimbali zinazochangia bei ya mafuta kupanda, pamoja na kutoa ruzuku ili kupunguza moja kwa moja gharama kwa wananchi.
“Duniani kumekuwa na habari kuhusu kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, hatua ambayo inahitaji kama nchi kuchukua hatua za haraka kushusha bei ya mafuta, sisi Chadema tuna msimamo wa kuitaka Serikali ipunguze tozo na kodi mbalimbali ili kushusha bei, pia itoe ruzuku kwenye mafuta ili kupunguza bei,” amesema Mnyika.