NIMEMSIKIA Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Francis Katabazi Mutungi, akieleza dhamira yake ya kutaka kuifuta au kusimamisha shughuli za kisiasa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaandika Philipo Mwakibinga … (endelea).
Kupitia barua yake ya tarehe 7 Mei mwaka huu, Mutungi anaituhumu Chadema kwa mambo mbalimbali, ikiwamo kutoa kauli anazoita, “…zinachochea mifarakano kwenye jamii.” Ameorodhesha mifano kadhaa.
Binafsi sina sababu ya kuingia kwa undani kujadili kilichosemwa na viongozi wa Chadema. Bali niishie tu kusema, kinachotajwa kuwa makosa ya Chadema, kimefanywa mara nyingi sana na viongozi waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kuanzia Dk. Bashiru Ally, aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho; Humphrey Polepole, Nape Nnauye, Paul Makonda, Amos Makalla, Mwigulu Nchemba, hadi viongozi wa mikoa na wilaya, kwa namna moja au nyingine, wameshatoa kauli zinazofanana na zile zinazodaiwa kutolewa na Chadema. Lakini hatujasikia wakiandikiwa barua au kuchukuliwa hatua.
Hivyo basi, kinachofanywa sasa na msajili wa vyama vya siasa, kwa maneno mengine, ni kukiri kwamba CCM na Serikali yake, kimeshindwa kufanya maridhiano ya kisiasa na upinzani, hususani Chadema.
Hii ni kwa sababu, maridhiano hayawezi kujengwa kwa kuondoa upande mmoja mezani. Yanajengwa kwa kuheshimu tofauti za kisiasa, haki za kikatiba na misingi ya demokrasia.
Wala vyama vya siasa haviwezi kufanywa kuwa adui wa taifa. Hii ni sauti ya sehemu ya wananchi. Ndio sababu taifa hili, kikaamua kufuata mfumo wa vyama vingi, takribani miaka 34 iliyopita.
Hata Katiba yetu inapingana na kinachoelezwa na Jaji Mutungi. Kinapingana na mikataba ya kimataifa na kinaingilia uhuru wa Chadema kufanya shughuli zake za kisiasa.
Mathalani, Ibara ya 18 (1) na (2) ya Katiba, zinaruhusu kuwapo uhuru wa maoni na uhuru kutafuta na kupokea habari bila ya kujali mipaka ya nchi.
Kwamba, kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Kwa muktadha huo, tishio lolote dhidi ya Chadema, linapalilia dhana kwamba serikali haiku tayari kwa maridhiano. Kwamba, inachokihubiri sicho inachokitenda. Inachokitenda sicho inachokiimba kwenye uso wa ulimwengu.
Kwamba, kutaka kukifuta chama kikuu cha upinzani nchini, kunaweza kuongeza mpasuko wa kisiasa nchini, kwa kuwa kunatuma ujumbe wa moja kwa moja kwa wananchi, kwamba ushindani wa kisiasa haukubaliki.
Chadema haitakiwi na kuwa na mawazo, ni kitisho badala ya kuwa mchango katika ujenzi wa taifa. Kupunguza imani ya wananchi kwa taasisi za dola, na kuharibu taswira ya nchi kimataifa.
Historia ya mataifa mbalimbali inaonyesha kuwa mataifa hayo yaliyofanikiwa kisiasa hayakuwahi kujenga umoja kwa kufungia au kufuta vyama vya upinzani, bali kwa kuimarisha mifumo ya haki, uchaguzi huru na maridhiano ya kweli.
Hata pale ambapo kulikuwa na migogoro mikubwa ya kisiasa, suluhisho lilikuwa ni maridhiano na mageuzi, si kufuta upinzani. Ikiwa kweli kuna nia ya kujenga Tanzania yenye umoja, amani na demokrasia imara, basi njia sahihi si kuifuta Chadema, bali kuhakikisha vyama vyote vinafanya siasa kwa mujibu wa sheria, kwa haki sawa na kwa kuheshimiwa mbele ya Katiba.
Demokrasia ya kweli hupimwa kwa namna serikali inavyovumilia ukosoaji na kuwapo uhuru wa kujieleza. Haipimwi kwa inavyozuia vyama kufanya kazi.