Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase
JESHI la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu wanne, wakazi wa Vikawe katika Manispaa ya Kibaha, kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kujeruhi na kusababisha vifo vya watu watatu mnamo tarehe 6 Mei 2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11 alfajiri, ambapo kundi la watu wanaodaiwa kwenda kuvunja nyumba za wakazi hao lilivamiwa, na kusababisha vurugu zilizopelekea watu 15 kujeruhiwa na watatu kupoteza maisha.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari, leo tarehe 14 Mei 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni sehemu ya upelelezi unaoendelea kuhusu migogoro ya ardhi iliyozua vurugu hizo huko Vikawe.
“Mnamo Mei 14, majira ya saa 10 jioni, askari walifanya msako mkali na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wanne wanaodaiwa kushiriki kikamilifu katika vurugu hizo ,kwa sasa wanahojiwa katika Kituo cha Polisi Kibaha kabla ya hatua zaidi za kisheria kuchukuliwa,” amsema Kamanda Morcase
Amewataja watuhumiwa waliokamatwa wametambuliwa kuwa ni Jackson Kilundwa (31): Fundi ujenzi David Mayengo (26) Mkazi wa Vikawe. Walter Urassa (33) ,Fundi ujenzi pamoja na Musa Tembo (34) Kuli wote wakazi wa Vikawe KIbaha.
Kuhusu hali ya majeruhi 13 waliokuwa wakipatiwa matibabu kutokana na vurugu hizo, Kamanda Morcase ameeleza kuwa baada ya matibabu kukamilika, mahojiano yalifanyika ambapo watu watano wameachiwa kwa dhamana huku wengine saba bado wanashikiliwa kituoni hapo wakisubiri kukamilisha taratibu zao za dhamana.
Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria na kutii sheria za nchi bila shuruti ili kuepuka majanga yanayoweza kuzitika.