MTANDAO wa watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), imesema kuwa licha ya kuwepo kwa vyombo vingi vya habari nchini Tanzania lakini hali ya uhuru wa habari kwa mwaka 2025/2026 imedorora.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Hayo yameainishwa na ripoti ya mwaka ya mtandao huo imewasilishwa jana tarehe 4 Mei 2026 na Mratibu wa Mtandao huo nchini Onesmo Olengurumwa, ambapo alieleza kuwa kushuka kwa uhuru wa habari nchi kunatokana na sababu za kiusalama, sheria.
“Mazingira ya vyombo vya habari yanaendelea kubanwa na sababu kadhaa muhimu, ikiwemo mfumo wa kisheria na kisera wenye vikwazo (changamoto za kikanuni), shinikizo za kiuchumi na kijamii, kujizuia kwa waandishi (self-censorship), ukosefu wa uhuru wa uhariri, vitisho vya kiusalama, kukamatwa kiholela, na mazingira yasiyofaa ya kisiasa,” alisema.
“Licha ya kuwepo kwa vyombo vingi vya habari nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na majukwaa ya mtandaoni, idadi hiyo haiakisi kwa usahihi kiwango halisi cha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza nchini, bali inaonesha hali ya kudhibitiwa kwa vyombo hivyo,” alisema Olengurumwa.
Amesema kuwa THRDC, inaamini kwamba vyombo vya habari huru, vinavyojitegemea na vyenye uwiano vina jukumu muhimu kama mlinzi wa maslahi ya umma kwa kuwafahamisha wananchi, kukuza uwajibikaji, kudumisha amani, kuimarisha utawala wa kidemokrasia na kuheshimu haki za binadamu.