RAIS wa Marekani, Donald Trump ameagiza kuanza kwa operesheni maalumu ya kijeshi ya majini kwa lengo la kusindikiza meli zilizokwama katika Mlango wa Hormuz kuanzia leo Jumatatu, akionya kuwa jaribio lolote la kuingilia operesheni hiyo litajibiwa kwa nguvu kubwa.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Hatua hiyo imekuja wakati meli zikiendelea kuzuiwa katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji kufuatia mvutano unaoendelea kati ya Marekani na Iran.
Trump amesema operesheni hiyo inalenga kuhakikisha usalama wa meli hizo, nyingi zikiwa zinamilikiwa na mataifa ambayo hayahusiki moja kwa moja na mzozo huo, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda biashara ya kimataifa na kusaidia wafanyakazi wa meli wanaokabiliwa na uhaba wa mahitaji muhimu baada ya siku kadhaa za usumbufu.
Hata hivyo, Iran imeonya kuwa uwepo wa kijeshi wa Marekani katika mlango huo utaonekana kama uvunjaji wa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili, hali inayoongeza hofu ya kuzuka upya kwa mivutano.