SIKU tatu baada ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kutangaza kuchunguzwa kwa watu waliobainika kufanya ubadhirifu kwenye malipo ya fidia za wananchi walioathirika kutokana na maeneo yao kutumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mamlaka ya kudhibiti rushwa na hujuma ya uchumi imetaka wahusika warudishe “haraka” fedha walizofisidi. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea)
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Zanzibar {ZAECA}, Ali Abdalla amesema wahusika wana muda wa “wiki mbili” za kurudisha fedha au mali walizopata kutokana na hatua ya serikali kufanya tathmini ya mali na kulipa fidia wananchi walioathirika.
“Mwananchi yeyote anayehusika katika ubadhirifu wa fedha au mali zinazohusiana na malipo ya fidia ya Serikali, kuhakikisha anarejesha fedha au mali hizo ndani ya kipindi hicho,” alisema Mkurugenzi wa Zaeca akitaja tarehe 14 Mei kuwa ndio siku ya kwanza ya muda huo wa wiki mbili na utakwisha ifikapo tarehe 28 Mei mwaka huu.
”Wote waliohusika waitumie fursa hii kurejesha fedha au mali husika kabla ya hatua za kisheria kufata,” alisema bila ya kutaja hao wahusika. Hata Rais Dk. Mwinyi hakutaja majina alipotangaza mbele ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi {CCM} aliowahutubia juzi akiwa ziarani kisiwani Unguja.
Dk. Mwinyi alieleza msimamo huo alipokuwa akizungumzia ripoti aliyokabidhiwa na Kamati aliyoiunda kufuatilia malalamiko ya wananchi waliodai kudhulumiwa malipo ya fidia kwa kuwepo udanganyifu wakati wa kazi ya tathmini ya mali za watu ambao maeneo yao yalitumika kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo wakati wa uongozi wake.
Akihutubia wanachama wa CCM alisema inasikitisha kuwa watendaji wa sekta ya ardhi nao wameguswa kwenye ripoti aliyokabidhiwa na kuahidi kuwa serikali haitamvumilia mtu yeyote, awe mtumishi wake au vinginevyo, ikibainika kweli amenufaika binafsi katika utaratibu wa serikali kufanya tathmini, kuandaa na kulipa fidia.
Aliitaka mamlaka hiyo kuchukua hatua zifaazo za kisheria kutokana na mambo mabaya yaliyobainishwa na Kamati ya uchunguzi. Kumekuwa na malalamiko mengi kwa muda mrefu sasa kuwa zoezi la tathmini na malipo ya fidia limegubikwa na udanganyifu kwa watumishi wa Idara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Fedha. Wakati akizindua Daraja la Juu eneo la Mwanakwerekwe, mapema mwaka huu, Rais Dk. Mwinyi alitaja kuhusu malalamiko hayo na ndipo alipoahidi kuunda kamati ya kufuatilia.
Siku hiyo, ilishuhudiwa mbele ya eneo alipohutubia wananchi, kuwepo bango kubwa lililoeleza kuwa familia husika haijalipwa haki yake ya fidia wakati sehemu ya nyumba yao ilivunjwa ili kupisha ujenzi wa daraja hilo. Ilielezwa kuwa familia hiyo ya kina Bwato, ilitishiwa na vyombo vya ulinzi na usalama ikitakiwa kuondoa bango hilo lakini ilisimama imara kutetea haki. Kutajwa kwa suala hilo na rais ilionesha alizipata taarifa mapema.
ZAECA imejitokeza sasa huku yenyewe ikikabiliwa na shutuma za ulegevu katika kutimiza majukumu yake. Baada ya kuanza kazi kwa nguvu kubwa, mara alipoingia madarakani Dk. Mwinyi, ikitangaza watuhumiwa ufisadi na uhujumu uchumi waliokamatwa, haikuthubutu kuruhusu waandishi wa habari kufika mahkamani kushuhudiwa wakisomewa mashtaka.
Na baadaye ilisita kabisa kutaja wa karibu na vyombo va habari hata pale ilipowafikisha mahkamani watuhumiwa.
Ilianzisha utaratibu wa kuwapeleka watuhumiwa kimyakimya huku wakifichwa wasionekane, na baadaye kuandika taarifa na kuisambaza kwa vyombo vya habari ikieleza nani waliofikishwa na kwa tuhuma gani. Mwandishi wa MwanaHALISI alikuwa miongoni mwa wachache waliopinga utaratibu huo na alipotaka ashuhudie mwenyewe wakifikishwa mahkamani, haikuwezekana. Hatimaye aliiarifu Idara ya Mawasiliano ya Mamlaka, iache kumtumia taarifa wakirudi mahkamani.
Hata hivyo, bado ZAECA inaendelea na utaratibu wake wa “usiri” inapofikisha watuhumiwa mahkamani.