MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania , imefanikiwa kukamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini kinyume na taratibu za kisheria jijini Dar es Salaam.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kemikali zilizokamatwa ni Cyclohexanone zenye ujazo wa lita 16,048 pamoja na Extra Neutral Alcohol (ENA) zenye ujazo wa lita 50,000. Aidha, magari mawili yaliyokuwa yakihusishwa na usafirishaji wa kemikali hizo yanashikiliwa, huku watuhumiwa wawili wakiwa tayari wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kemikali hizo ni halali kwa matumizi mbalimbali ya viwandani, kitabibu, kilimo, ujenzi,madini pamoja na tafiti za kisayansi, lakini wahalifu huzitumia vibaya kwa kuzichepusha kutoka katika matumizi halali na kuzitumia kutengeneza dawa za kulevya.
DCEA imeongeza kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali bashirifu ili kuzuia uchepushwaji wake na kuhakikisha zinatumika kwa matumizi halali pekee.