Tundu Lissu akiwa mahakamani
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Boniface Mwabukusi, ametoa rai kwa mhimili wa Mahakama nchini kuharakisha usikilizwaji wa kesi zinazomkabili mwanasiasa Tundu Lissu, akisisitiza kuwa mahakama haipaswi kuwa sehemu ya “kupaki” mashauri kwa muda mrefu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo 11 Mei 2026, jijini Dar es Salaam, Mwabukusi amesema kuwa ingawa TLS inaheshimu uhuru wa mahakama na inapinga shinikizo lolote kutoka nje, ni jukumu la chama hicho kuikumbusha mahakama kufuata miongozo yake ya kuharakisha upatikanaji wa haki.
Mwabukusi ameeleza kuwa kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pamoja na mashauri yaliyopo Mahakama ya Rufaa, yanapaswa kusikilizwa kwa uharaka ili haki ionekane kutendeka kwa wakati.
“Rai yetu kama Chama cha Wanasheria Tanganyika ni kwamba haki itendeke kuhusu Tundu Lissu; kesi yake isikilizwe na kama hawana nia ya kuisikiliza wamuachie.
“Mahakamani sio sehemu ya kupaki kesi kama Jaji Mkuu alivyoeleza juu ya Mahakama za Rufani. Tunataka kuona tafsiri ya miongozo ya mahakama ikifanya kazi kwenye kesi kama hizi,” amesema Mwabukusi.
Rais huyo wa TLS amefafanua kuwa miongozo ya mahakama imeweka taratibu za muda ambao kesi inapaswa kuchukua mpaka kukamilika, hivyo TLS haijatenda kosa kuikumbusha mahakama kutimiza wajibu wake na kuwa kuchelewesha kwa mashauri hayo kunatoa taswira ya kuingiliwa kwa misingi ya haki.
Aidha, Mwabukusi amehitimisha kwa kusema kuwa TLS itafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa rai hiyo ili kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria hazitumiwi kama kisingizio cha kuchelewesha haki ya raia.