Jumanne Muliro, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limethibitisha kupokea taarifa ya kifo cha mwanamke aliyefahamika kwa jina la Aisha Miraji, mkazi wa Nzasa Temeke, ambaye mwili wake ulipatikana kwenye maji eneo la daraja la Salender, Ilala, mnamo tarehe 11 Mei 2026 majira ya saa 4:30 asubuhi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya polisi, mwili wa marehemu haukuonekana kuwa na jeraha lolote. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Aisha alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili tarehe 10 Mei 2026 akiwa pamoja na wazazi wake kabla ya kupotea ghafla eneo la hospitali hiyo.
Wazazi wa marehemu wameeleza kuwa mtoto wao alikuwa akisumbuliwa na changamoto za kiafya kwa kipindi tofauti tofauti ndani ya miaka mitano iliyopita.
Baada ya kupotea akiwa Muhimbili, juhudi za kumtafuta zilianza hadi mwili wake ulipopatikana eneo la Salender siku iliyofuata.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira halisi yaliyopelekea kifo hicho