WAKAZI wa maeneo mbalimbali wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani wanatarajiwa kukumbwa na ukosefu wa huduma ya maji kwa wastani wa saa 10 kesho Jumapili 10 Mei 2026, kufuatia matengenezo kinga ya miundombinu ya umeme. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea
Taarifa iliyotolewa kwa umma na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) huduma hiyo itaathirika kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kwa wananchi wanaohudumiwa kupitia mitambo ya Ruvu Chini wilayani Bagamoyo na Ruvu Juu wilayani Kibaha.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuruhusu matengenezo ya miundombinu ya umeme katika kituo cha kupooza umeme Mlandizi, hatua inayotarajiwa kusaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa muda mrefu.
Maeneo yatakayoathirika kupitia mtambo wa Ruvu Chini ni pamoja na Bagamoyo, Mapinga, Bunju, Tegeta, Kunduchi, Mbezi Beach, Kawe, Lugalo, Makongo, maeneo ya vyuo vikuu vya UDSM na Ardhi, Mwenge, Mikocheni, Masaki, Oysterbay, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni na Kigogo.
Mengine ni Chang’ombe, Kurasini, Kigamboni, Airport, Kiwalani, Buguruni, Vingunguti, Ilala na katikati ya jiji.Kwa upande wa mtambo wa Ruvu Juu, maeneo yatakayokosa huduma ni pamoja na Ruvu Darajani, Vigwaza, Mlandizi, Mbwawa, Visiga, Maili 35, Kongowe, Soga, Miembe Saba, Mbezi, Kimara, Tabata, Segerea, Kinyerezi, Kisukuru, Bonyokwa, Msigani, Ubungo, Ukonga, Gongo la Mboto, Pugu na Kisarawe.