KAMATI Ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya, imeeleza kusikitishwa dhidi ya maamuzi ya Serikali ya Tanzania kuahirisha mara kwa mara ujio wa kamati hiyo, iliyokuwa imepanga kufika Tanzania tangu mwezi wa pili Mwaka huu kwaajili ya kutekeleza majukumu yake ya kukagua hali ya demokrasia na haki za binadamu nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Katika tamko lililotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mounir Satouri ameeleza kuwa kitendo cha mamlaka za Tanzania kuendelea kuomba kuahirishwa kwa ziara ya ujumbe huo ni sawa na kukataa kuipokea kamati hiyo.
“Katika muktadha huu, tunasikitishwa na ukosefu wa utayari wa mamlaka za Tanzania kushiriki katika mazungumzo ya nia njema, hasa wakati kukiwa na hali inayozorota ya haki za binadamu na ukandamizaji wa upinzani wa kidemokrasia.”
“Licha ya vikwazo vya sasa, chombo chetu cha kibunge kitatafuta njia zote zilizopo ili kufuatilia kwa karibu maendeleo ya haki za binadamu, demokrasia, na utawala wa sheria nchini Tanzania na kutathmini athari zake katika maendeleo ya baadaye ya uhusiano wa Nchi hiyo na Umoja wa Ulaya” amesema Satouri.
Mkutano wa Marais wa Bunge la Ulaya wa tarehe 20 Novemba 2025 uliidhinisha ujumbe wa kamati ndogo ya haki za binadamu kuja Tanzania. Wakilenga masuala yanayohusu haki za binadamu, demokrasia, na utawala wa sheria, kulingana na majukumu ya kamati hiyo.
Wabunge wa Ulaya walikusudia kufuatilia maazimio ya Bunge la Ulaya yanayohusu Tanzania yaliyopitishwa mnamo Novemba 2025, kushirikiana na serikali, bunge, asasi za kiraia na wadau wa kimataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu, kutembelea Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu jijini Arusha, na kukagua miradi inayofadhiliwa na EU katika nyanja ya haki za binadamu.
Kulingana na taarifa ya Umoja wa ulaya kwa Vyombo vya habari, Ujumbe huo awali ulipanga kuja Februari.
Hata hivyo, mamlaka za Tanzania ziliomba uahirishwe hadi tarehe ya baadae ili kutoa muda kwa tume ya kitaifa ya uchunguzi inayochunguza ghasia za uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba 2025 kukamilisha kazi yake.