RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, anakabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa baada ya Mahakama ya Katiba kuamua kuwa Bunge lilikiuka Katiba kwa kuzuia mchakato wa kumuondoa Madarakani mwaka 2022.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Mwanasiasa mashuhuri wa Upinzani Julius Malema alimtaka Ramaphosa kujiuzulu mara moja kufuatia uamuzi huo wa Mahakama.Kesi hiyo iliwasilishwa na Vyama vya Upinzani, vikiwemo Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF).Uamuzi wa Mahakama unaweza kufungua njia ya kura mpya ya kutokuwa na imani na Rais katika Bunge la Afrika Kusini.
Mwaka 2022, jopo la wataalamu wa Sheria lilisema Ramaphosa alikuwa na maswali ya kujibu baada ya zaidi ya Dola 500,000 kuibwa katika nyumba yake ya mashambani. Fedha hizo ziliripotiwa kuwa zilikuwa zimefichwa ndani ya sofa.
Tuhuma hizo ziliibua maswali kuhusu chanzo cha fedha hizo, lakini Ramaphosa alikanusha kufanya kosa lolote.Wakati huo, juhudi za kumuondoa Madarakani zilishindikana kutokana na chama chake cha ANC kuwa na wingi mkubwa bungeni.Hata hivyo, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, ANC ililazimika kuunda Serikali ya Muungano baada ya kupoteza wingi wa moja kwa moja.
Msemaji wa ANC, Mahlengi Bhengu, alisema chama hicho kinaheshimu uamuzi wa Mahakama na Viongozi wake watakutana kujadili hatua zinazofuata.Akizungumza nje ya mahakama, Julius Malema alisema Ramaphosa anapaswa kujiuzulu na kuanza kujitetea dhidi ya mchakato unaoweza kumuondoa madarakani.