IMERIPOTIWA kuwa watu wasiojulikana wamevamia eneo la Vikawe (Lupaso), Kata ya Pangani wilayani Kibaha na kusababisha mauaji ya watu wawili huku wakijeruhi 14 kufuatia mgogoro wa ardhi uliotokea katika eneo hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Abubakar Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, akizungumza na waandashi habari ofisini kwake leo tahere 6 Mei 2026, amethibitisha kutokea tukio hilo la uvunjifu wa amani na kusababisha vifo na majeruhi.
Amesema watu wasiojulikana walifika katika eneo hilo wakidaiwa kuwa na lengo la kuwaondoa wakazi wanaodaiwa kuvamia ardhi inayomilikiwa kihalali, hali iliyosababisha vifo vya watu wawili .
Kunenge ameeleza kuwa majeruhi wote wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika hospitali hiyo.
Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo, mmiliki halali wa eneo pamoja na waliowatuma watu hao kwenda kuwaondoa wakazi.
Vilevile, amewataka wananchi kujiepusha na kujichukulia sheria mkononi na uvamizi wa maeneo yasiyo yao.
Pia wamiliki wa ardhi wanapaswa kufuata taratibu za kisheria wanapokumbana na migogoro, ikiwemo kufikisha suala hilo katika mabaraza ya ardhi au mahakamani.
Pia, endapo kuna amri ya mahakama ya kubomoa nyumba, washirikishe vyombo vya dola badala ya kuchukua hatua binafsi,” amesisitiza Kunenge.
Kwa upande wake, mkazi wa Chato, Vikawe, Kidawa Hamidu, ameiiomba Serikali ya Mkoa pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo ili haki ipatikane kwa pande zote.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Siaely Moshi, amethibitisha kupokea majeruhi hao sanjali na vifo vya watu wawili wanaume, akieleza kuwa majeruhi kumi wanaendelea kupatiwa matibabu na wengine wanaendelea vizuri.