KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) imelaani vikali kuibuka kwa matukio ya kuokotwa kwa miili ya watu waliopoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha nchini.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …(endelea).
Kupitia tamko lake rasmi, LHRC imeeleza kusikitishwa na kuongezeka kwa matukio hayo, huku ikionesha wasiwasi mkubwa juu ya ukimya wa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo havijatoa ufafanuzi wa kutosha kwa umma kuhusu chanzo cha matukio hayo.
Shirika hilo limeeleza kuwa hali hiyo inazua hofu na taharuki miongoni mwa wananchi, na kusisitiza kuwa ni wajibu wa mamlaka husika kuhakikisha usalama wa raia pamoja na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.
Aidha LHRC imesisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka, za uwazi na zenye uwajibikaji ili kuchunguza matukio hayo kwa kina na kuwabaini wahusika.
LHRC imekumbusha kuwa kulinda haki ya kuishi ni jukumu la msingi kwa kila dola, na kwamba kila Mtanzania ana haki ya msingi ya kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na mauaji yasiyoeleweka.