WAZIRI Mkuu wa Uingereza na kiongozi wa chama cha Labour, Keir Starmer, ametangaza kujiuzulu madaraka yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Starmer anasema, tayari amemjulisha Mfalme wa taifa hilo, kuhusu hatua yake hiyo, leo asubuhi na kukitaka chama chake, kuweka ratiba na uteuzi wa kiongozi mpya.
Kwa mujibu wake, kiongozi mpya wa Lebour anapaswa kupatikana tarehe 9 Julai mwaka huu, kabla ya Bunge kurejea na mikutano yake mwezi Septemba.
Hata hivyo, Starmer ataendelea kuwa waziri mkuu hadi kiongozi mpya atakapopatikana.
Vyanzo vya taarifa vinasema, Starmer amelazimika kujiuzulu kama kiongozi wa chama tawala cha Labour, baada ya shinikizo kubwa la kisiasa.
Uamuzi huo umefuatia kuongezeka wito kutoka kwa wanachama wa chama chake na wabunge wanaotaka mabadiliko ya uongozi, ili kufufua matumaini ya serikali ambayo yamekuwa yakidorora.
Katika taarifa yake, Starmer alikiri kuwa muda umefika kwa chama hicho kuanza ukurasa mpya, akisisitiza umuhimu wa kuwapo uongozi mpya unaoweza kurejesha imani ya wananchi.
Kabla ya kutangaza kujiuzulu, Starmer alisema alirithi chama cha Labour, “kilichofilisika kisiasa, kifedha na kimaadili.” Alikibadilisha chama hicho kwa “kung’oa sumu ya chuki dhidi ya Wayahudi.”
Anasema, aliambiwa “mara kwa mara” kwamba karamu “ilikuwa imeisha,” lakini anasema “alithibitisha kuwa watu hao walikuwa na makosa.”
Starmer aliingia madarakani baada ya kuiongoza Labour kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Julai 2024.
Hata hivyo, ndani ya kipindi cha miaka miwili tu, umaarufu wake binafsi pamoja na chama chake umeshuka kwa kiwango kikubwa, jambo lililozua wasiwasi miongoni mwa wafuasi na wadau wa siasa.
Kujiuzulu kwake kunahusishwa kwa karibu na ushindi wa Andy Burnham katika uchaguzi mdogo uliofanyika wiki iliyopita.
Burnham, aliyekuwa meya maarufu wa Greater Manchester, alikuwa ameonyesha nia ya kumkabili Starmer katika kinyang’anyiro cha uongozi wa Labour — jambo lililoongeza shinikizo la kuachia ngazi.
Wachambuzi wa kisiasa wanaamini kuwa ushindi huo wa Burnham uliashiria mabadiliko ndani ya Labour na kuonesha wazi kuwa wanachama wengi walikuwa wakitamani uongozi mpya.
Sasa macho yote yanaelekezwa kwa mchakato wa uchaguzi wa kiongozi mpya wa chama, ambao unatarajiwa kuamua hatma ya Labour na mwelekeo wa kisiasa wa serikali ya Uingereza katika kipindi kijacho.
Endelea kufuatilia MwanaHALISI.