MAHAKAMA Kuu ya Kenya imethibitisha uamuzi wa Bunge la Taifa na Seneti wa kumuondoa madarakani aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ikisema kuwa mchakato huo ulifanyika kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya nchi hiyo.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Katika hukumu iliyotolewa Jumatatu, 8 Juni 2026, jopo la majaji watatu lililojumuisha Eric Ogolla, Anthony Mrima na Freda Mugambi, lilibaini kuwa wabunge na maseneta walikuwa na msingi wa kisheria wa kuanzisha na kuendeleza mchakato wa kumuondoa Gachagua madarakani mwezi Oktoba 2024.
Mahakama ilikataa ombi la kufuta uamuzi wa Seneti, hatua inayomaanisha kuwa kuondolewa kwake madarakani kunabaki kuwa halali kisheria.
Hata hivyo, majaji walieleza kuwa baadhi ya haki zake za kikatiba zilikiukwa wakati wa mchakato huo, na kuamuru alipwe fidia ya Shilingi za Kenya milioni 50, sawa na takriban Shilingi bilioni 1 za Tanzania.
Awali, Gachagua alikuwa ameomba zaidi ya Shilingi za Kenya milioni 80 pamoja na mafao ya kustaafu, akidai kuwa mchakato wa kumwondoa ulikuwa wa kisiasa, ulikiuka Katiba na haukumpatia fursa ya kutosha ya kujitetea.