CHAMA cha Watu Wenye Ualbino Mkoa wa Mwanza (TAS) kimetoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto wenye ualbino kuhakikisha wanaendelea kuwapatia vifaa kinga vinavyowasaidia kujilinda dhidi ya miale mikali ya jua katika kipindi hiki cha likizo ya shule. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Wito huo umetolewa na Katibu wa TAS Mkoa wa Mwanza, Angelina Chuma, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Uelewa kuhusu Ualbino ngazi ya mkoa yaliyofanyika wilayani Misungwi. Amesema kuwa wakati watoto wanaporejea nyumbani kwa likizo, wazazi wanapaswa kuzingatia afya na utunzaji wa ngozi zao ili kuwakinga dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na jua.
Aidha, Chuma ametoa rai kwa mashirika mbalimbali kuendelea kushirikiana na jamii kwa kutoa vifaa kinga na msaada unaohitajika kwa watu wenye ualbino.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walioshiriki maadhimisho hayo wameishukuru ActionAid pamoja na Desk and Chair Foundation kwa msaada wanaoendelea kutoa, huku wakiiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Naye Mwakilishi wa ActionAid, Yusuph Bwango, ameeleza umuhimu wa Wiki ya Uelewa kuhusu Ualbino inayoadhimishwa duniani kote, akisisitiza jamii kuendelea kuwalinda, kuwathamini na kuwatunza watu wenye ualbino.