Zitto Kabwe
KIONGOZI Mstaafu wa ACT-Wazalendo na Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Zitto Kabwe, ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuachana na kesi inayomkabili Tundu Lissu bila masharti yoyote, akisema hatua hiyo italiletea taifa manufaa makubwa kuliko hasara zinazodhaniwa na baadhi ya mamlaka. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza wakati akihojiwa na Clouds Media, Zitto amesema kuachiwa kwa Lissu kutakuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha haki za wananchi na kurejesha matumaini ya kisiasa nchini.
“DPP akiachana na kesi ya Lissu bila masharti yoyote nchi itafaidika zaidi kuliko madhara ambayo wao wanayawaza,” amesema Zitto.
Amesema suala la Lissu ni sehemu tu ya changamoto nyingi zinazohusu haki za wananchi katika kesi mbalimbali, hivyo mamlaka zinapaswa kuchukua hatua sahihi.
Aidha, ameeleza kuwa ni muhimu Lissu akaachiwa ili arejee kufanya majukumu yake, kuungana na familia yake, pamoja na kushiriki kikamilifu katika michakato ya kulisukuma taifa kusonga mbele.
“Taifa letu halifaidiki kwa namna yoyote ambayo Lissu anaitumia akiwa ndani ya gereza. Muachilieni Lissu,” amesema.