Mkuu wa Utawala tawi la JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewaita vijana 60,000 waliomaliza kidato cha sita ili kujiunga na mafunzo ya lazima (kwa mujibu wa sheria). Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Idadi hiyo imekuja kufuatia kauli ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa aliyotoa hivi karibuni kwenye bajeti yake akisema wameongeza kutoka washiriki 40,000 hadi 60,000.
Hata hivyo, JKT wamesema mwelekeo wa mbeleni ni kuhakikisha vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wanakwenda moja kwa moja kwenye makambi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi 28 Mei 2026 kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele,
Mkuu wa Utawala tawi la JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana hao wataanza kuripoti 1 Juni 2026.
Brigedia Jenerali Mabena amesema mpango huo unagusa vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026, kutoka shule zote za Tanzania Bara na visiwani.
“Sanjari na wito huo, JKT limewapangia makambi watakaokwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti kambini kuanzia 1 hadi 7 Juni 2026,” amesema Mabena.
Ametaja baadhi ya Makambi ya JKT waliyopangiwa ni Rwamkoma, Mara, Msange, Tabora, Ruvu, Kibiti, Mpwapwa, na Makutupora.
Makambi mengine ni Mafinga, Iringa, Male,Ruvuma, Mgambo, Maramba, Tanga, Makuyuni JKT na Oljoro, Arusha, Bulombora, Kagera, Kanembwa, Mtabila, Kigoma, Itaka, Songwe, Luwa, Milundikwa, Rukwa, Nachingwea, Lindi na Chuo cha Uongozi JKT (CUJKT) Kimbiji – Dar es Salaam.