Rais Samia Suluhu Hassan
RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu yameiacha nchi na funzo kubwa kuhusu namna ya kushughulikia vitisho vya kiusalama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza leo 28 Mei 2026 jijini Dar es Salaam, katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya maafisa na wakaguzi wasaidizi wa Polisi, Rais Samia amesema kuwa Tume ya Uchunguzi ya matukio hayo ilibainisha kuwa sehemu ya changamoto zilizojitokeza zilichangiwa na desturi na namna Watanzania walivyozoea kuamini kuwa nchi ni ya amani muda wote.
Amesema tabia hiyo ya kutochukulia vitisho kwa uzito inawafanya baadhi ya watu kudhani hakuna lolote kubwa linaloweza kutokea, lakini matukio ya uchaguzi huo yalionesha umuhimu wa kuwa makini.
“Tume ya Uchunguzi ilisema kwamba labda kwa sababu ya uzoefu wetu, mila na desturi kwamba Tanzania ni nchi ya amani, tunapuuza vitisho. Tunaona kama hakuna kikubwa kinaweza kutokea. Lakini yaliyotokea yametupa funzo,” amesema.
Aidha, amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua walizochukua kudhibiti haraka na kwa ufanisi hali ya sintofahamu iliyojitokeza siku hiyo.