Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo
WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema imesikitishwa na taarifa za upotoshaji kuhusu matamshi yasiyo sahihi yanayosambazwa kupitia Mitandao ya Kijamii kufuatia Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo iliyowasilishwa Bungeni Jijini Dodoma 26 Mei 2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Miongoni mwa mijadala iliyoibuka mitandaoni ni kuhusu msimamo wa Serikali juu ya kutokuingiliwa katika mambo ya ndani ya Nchi.
Katika taarifa iliyotolewa leo 28 Mei 2026 na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara hiyo imesema taarifa zinazosambazwa mitandaoni zimepotosha maudhui halisi ya hotuba hiyo kwa makusudi kwa lengo la kuleta mkanganyiko kwa Umma na kuathiri taswira ya Nchi pamoja na misingi ya Diplomasia, Uhuru na Mshikamano wa Kitaifa.
Kutokana na hali hiyo, Wizara imesema itaendelea kutoa ufafanuzi rasmi kupitia Vyombo vya Habari na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano ili kuhakikisha Wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye muktadha stahiki wa Serikali kuhusu masuala yaliyojadiliwa katika hotuba hiyo.
“Wizara inatoa wito kwa watumiaji wa Mitandao ya Kijamii, wadau wa Habari na Wananchi kwa ujumla kutumia Uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia Weledi, Maadili, Sheria za Nchi pamoja na wajibu wa kulinda amani, mshikamano na heshima ya Taifa letu,” imeeleza taarifa hiyo.
Bajeti hiyo iliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.