KITUO cha Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kimependekeza tarehe 29 Oktoba kila mwaka iwe siku ya kitaifa ya kumbukizi ya matukio yaliyotokea tarehe 29 Oktoba 2025 ili kuwakumbuka walioathirika na waliofariki dunia.Anaripoti Zakia Nanga,Dar es Salaam … (Endelea)
Kimesema kumbukumbu hiyo isukume Taifa kuweka mikakati ya kuzuia kujirudia kwa vifo,majeruhi na ukiukwaji wa haki za binadamu uliotokea siku hiyo ya uchaguzi na zilizofuata.
Katika taarifa yake iliyotolewa tarehe 23 Oktoba 2026, THRDC imesema siku hiyo inapaswa kuwa zaidi ya maombolezo kwa kuwa fursa ya kutafuta ukweli,kutenda haki,kuimarisha uwajibikaji na kujenga mshikamano wa kitaifa.
Kituo hicho kimesisitiza kuwa kumbukizi hiyo inapaswa kuongozwa na falsafa ya “Yasijirudie Tena”(Never Again),huku juhudi za maridhiano zikienda sambamba na uchunguzi wa kuaminika na uwajibikaji pale makosa yatakapothibitishwa.
Aidha THRDC imependekeza kutathminiwa kwa mifumo ya ulinzi wa raia na uwajibikaji wa vyombo vya usalama na kuhifadhi kumbukumbu za matukio hayo kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Kituo hicho kimetolea mfano Rwanda,ambayo huadhimisha kumbukuzi ya mauaji ya Kimbari kuanzia 7 Aprili na Afrika Kusini ambayo huadhimisha siku ya Haki za Binadamu 21 Machi,inayohusishwa na mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1960.
THRDC imependekeza kumbukizi ya kwanza kufanyika 29 Oktoba 2026,kwa kushirikisha familia za wathirika, taasisi za umma,viongozi wa dini,asasi za kiraia na wananchi katika ngazi za kitaifa,mikoa na wilaya.
Pia kituo hicho kinapendekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa kuhifadhi kumbukumbu za matukio hayo na hatimaye kujenga makumbusho rasmi huku tathmini ya kila mwaka ikifanyika kuhusu utekelezaji wa hatua za kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo.
Kaulimbiu iliyopendekezwa na kituo hicho ni “Kumbukizi,Ukweli,Haki,Uwajibikaji na auponyaji,Kamwe Yasijirudie Tena.”
Mwisho.