CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kuwa Mkuu wa Gereza Kuu la Ukonga amekaidi amri ya Mahakama Kuu ya kumruhusu Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama hicho kuzungumza na mawakili wake bila kusikilizwa na askari wa gereza.
Lissu anashikiliwa katika gereza hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa akikabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dodoma iliyoketi katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, tarehe 16 Oktoba mwaka huu, ilipiga marufuku maofisa wa magereza kusikiliza mazungumzo ya Lissu na mawakili wake.
Uamuzi huo katika shauri la kikatiba Na. 7300/2026 lilikuwa mbele ya jopo la majaji watatu liliongozwa na Kaimu Jaji Kiongozi Amir Mruma, akishirikiana na Jaji Dk. Angelo Rumisha na Jaji Dk. Evaristo Longopa.
Mahakama iliwataka maofisa wa magereza kukaa sehemu wanayoweza kuona na sio kusikiliza mazungumzo ya faragha ya mtuhumiwa na wakili wake.
Leo tarehe 24 Oktoba 2026, Dk. Rugemeleza Nshala, Mwanasheria Mkuu wa Chadema amesema kuwa maofisa wa magereza wameendelea na tabia yao ya kutaka kusikiliza mazungumzo ya Lissu na mawakili wake tangu kutolewa kwa amri hiyo.
MwanaHALISI online, limeshindwa kuwapata viongozi wa gereza la Ukonga kuthibitisha madai hayo ya kukiuka amri ya mahakama kutokana na simu zao kuita pasi majibu.
Kwa mujibu wa Dk. Nshala baada ya hukumu hiyo kutolewa mawakili wao walikwenda gerezani Ukonga kwa ajili ya kumuona Lisssu na wakaambiwa utaratibu ni ule ule.
Dk. Nshala amesema kuwa Lissu ametangaza kuwa kuanzia keshokutwa ataanza mgomo wa kula.
“Kuanzia Jumatatu tarehe 26 ataanza mgomo wa kula…Jana nimekwenda Ukonga saa saba mchana nikaitwa pembeni kwanza na mwanasheria wa gereza akaniambia Lissu amesema hawezi kuzungumza na wewe kwa sababu utaratibu ni uleule kwa hiyo wewe urudi nikamwambia nataka nimsikie mwenyewe.
“Nikamwambia Mwanasheria wa si kuna amri Mahakama mbona hamuifuati akanijubu kuwa ni maagizo ya kutoka juu”
Baadaye mwenyekiti akaletwa akasema hayupo tayari kuzungumza nami ikiwa mazungumzo yanasikilizwa, gereza linavunja sheria nami nikisema hivyo nitakuwa nimevunja sheria,”amesema Dk. Nshala.
John Mnyika Katibu Mkuu wa Chama hicho amesema kuwa Lissu amekosa imani na magereza ndio maana ya kuanza mgomo huo.
“Kama magereza haiheshimu amri ya mahakama kwa waziwazi, je hicho chakula anachopewa na hao kitakuwa na usalama kiasi gani? Huu ndio wasiwasi wa Mwenyekiti Lissu,”.
Amesema kuwa hatua ya Lissu gerezani ni kupaziwa sauti ili kuhakikisha anakuwa salama, usalama wa kupata chakula, na usalama wa kupata uwakilishi wa mawakili.
“Watu waliokwenda gerezani Jumamosi na Jumapili iliyopita wamezuiwa kwenda kumuona Lissu kwa madai wanaotakiwa kumuona ni ndugu zake peke yake.”
“Lissu ametoa wito kwa Watanzania kuonesha mshikamano kwake kuanzia tarehe 26 Oktoba kufikisha ujumbe kwamba tunataka haki za Lissu, wafungwa walioko magerezani, haki ya kulindwa kwa sheria na Katiba na haki ya kulinda amri za Mahakama” .
Mwisho.