LEO Tanzania inadhimisha miaka 25 tangu kifo cha aliyekuwa Baba wa Taifa Julius Nyerere, kilichotokea katika hospitali ya St. Thomas nchini Uingereza tarehe 14 Oktoba, 1999. Anaandika Salehe Mohamed …(endelea).
Kila mwaka Tanzania inakumbuka kifo chake kwa namna tofauti ili kuenzi kazi njema aliyoifanya kwa taifa.
Kiongozi huyu alitawala kwa miaka 24 kabla ya kung’atuka mwaka 1985. Katika utawala wake alipiga vita ubaguzi, ufisadi, rushwa, umasikini na matumizi mabaya ya madaraka.
Alihimiza umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali kabila, dini na eneo analotokea mtu. Aliamini binadamu wote ni sawa na Watanzania wote ni ndugu. Aliamini vyombo vya dola ni mali ya umma si Chama Cha Mpinduzi (CCM), kama tulivyoambiwa.
Leo hii tunapoadhimisha miaka 27 tangu kifo chake ni kweli tu wamoja? Siasa, dini, umasikini na ukabila havijatufanya tubaguane? Rasilimali tulizonazo zinanufaisha wengi au wachache?
Tujiulize leo hii tunapofanya sherehe za kumbukumbu yake huku tukifuja mabilioni ya fedha za walalahoi, hapo tutakuwa tunamuenzi au tunamdhihaki mwasisi wa taifa letu?
Yale matabaka ya watawala na watawaliwa aliyoyakataa tunayo au hatuna? Familia za viongozi hazina tofauti kubwa na wale wanaowaongoza? Watoto, ndugu na jamaa zao wanapendelewa au wanapata fursa sawa katika ajira, fursa za kiuchumi na kielimu?
Majibu ya maswali haya tunayo wenyewe na ndiyo yanapaswa kutuongoza katika tathimini ya miaka 27 bila ya hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Leo hii watoto wa viongozi ndiyo wenye sauti zaidi kuliko hata watumishi wa umma. Si tumeona mke na mtoto waziri anatukana askari na hafanywi chochote?
Mwalimu Nyerere alitushawishi tuukubali mfumo wa vyama vingi kwa kuwa unaimarisha demokrasia na kukuza wigo wa mtu kuchagua au kuchaguliwa, je leo hii chama alichokiasisi wanalienzi hili kwa vitendo?
Chama alichokiasisi kinakubali kushindwa kwenye sanduku la kura au linatumia mali zake (vyombo vya dola) kuhakikisha vinashinda hata sehemu walikoshindwa. Alituambia rushwa ni adui wa haki na tumuogope kama ukoma mtu anayetumia fedha kuingia madarakani. Leo hii tunambiwa mkono mtupu haulambwi. Ukitaka kura toa kula.
Tunatimiza miaka 27 bila ya uwepo wa Nyerere huku tukiwa tumeikumbatia rushwa na imetuganda kama ruba, tuna sababu za kujivunia sisi ni wafuasi wake?

Alitusihi tuachane na wanasiasa wenye tabia za ‘kimalaya’ za kuwa tayari kuuza utu na heshima yao ilmradi wapate fedha tu. Kuna watu wako tayari kutoa vibali vya kuweka bandari kavu hata kwenye eneo la jeshi bila kujali athari siku ikitokea mabomu yamelipuka.
Fedha sasa ndiyo kigezo cha kuchagua na kuchaguliwa, yaani mkono mtupu haulambwi. Ofisi za umma zimegeuzwa miradi binafsi, anayechaguliwa au kuteuliwa tunamsifu ‘ameula.’
Huyu aliyeingia madarakani kwa kununua uongozi ndiye hufanya juu chini kurudisha fedha zake kupitia kandarasi, miradi au zabuni mbalimbali halafu tunalalamikia kusuasua kwa maendeleo.
Chama alichoshiriki kukiasisi mwaka 1977 ndicho kinachoongozwa kwa kufanya vitu vinavyodumaza demokrasia, ndicho kinanunua watu kwa khanga, kofia, vilemba na fedha. Badala ya kuogopwa kama ukoma kinashangilia na kukimbiliwa.
Kinakimbiliwa si kwa sababu kinavutia watu bali hofu ya kushughulikiwa watu wasiokubaliana nacho. Siasa zimekuwa uadui. Nyerere uliyesema CCM si mama wala baba yako kwa maana kwamba unaweza kukihama siku kikifanya tofauti leo hii ni ‘mbele kwa mbele.’
Chama tawala ulichokiacha na kutumia nguvu kubwa kukemea wala rushwa na kuwasihi watu wachague watu wadilifu leo hii, kila unapofika uchaguzi iwe ndani ya chama hicho au nje bila kuwa na fedha utaula wa chuya. Sasa ni biashara ya kuuza na kununua.
Kile chama kilichosifika kwa ubora wa sera, ilani na wagombea sasa hivi ndicho kinasifika kwa kubagua, kutengeneza makundi kutumia rushwa na kulindana.
Uwajibikaji na kuwajibishwa si lugha yenye kuelewaka tena. Ni kila mtu ale kulingana na urefu wa kamba yake.
Sasa hivi kila kiongozi akisimama anamwaga sifa Rais kafanya hiki, kafanye kile atafanya kile halafu hawatuambii wenyewe wamefanya nini? Yaani kila kitu hivi sasa kinamsubiri Rais.
Yaani ile Tanzania ambayo Nyerere aliiacha akihimiza watu walipe kodi na zitumike kujenga nchi, sasa kodi zinafanywa miliki ya mkuu wa nchi hivyo serikali inapozitoa tena kwa kupitia Bunge bado inaonekana zimetoka Ikulu.
Mwalimu Nyerere hakuacha Tanzania wala CCM ya kujikomba kwa viongozi, aliamini kwenye ukosoaji na kujisahihisha pale tulipokosea.
Wakosoaji iwe ndani au nje ya chama na serikali wameamua kufunga midomo yao si kwamba tunakwenda vizuri bali kunusuru vichwa vyao na familia. Hii ndiyo Tanzania ya sasa.
Nyerere ulitueleza kuwa utawala wako haukuwa wa malaika na kuna maeneo mlikosea ndiyo maana ulitutaka tuchukue mazuri na kuyaacha mabaya, leo hii wapo baadhi ya viongozi wanajiona malaika na ukiwakosoa cha moto utakiona wewe na familia yako.
Ukoloni na ubaguzi tulioupinga kwa nguvu zetu zote na kuwatimua wakoloni sasa umerudi kwa mlango wa nyuma tena ukiratibiwa na waliopewa dhamana ya kuongoza.
Tuna viongozi waliofilisika kifikra, matabaka ya walionacho na wasionacho yanazidi kuongezeka. Ubaguzi wa kidini, kikanda, kikabila unazidi kumea taratibu na wengine hawaoni aibu kujinasibisha nao.

Nyerere alituachia kilimo ni uti wa mgongo na siasa ni kilimo, leo hii kilimo kimegeuzwa ngazi ya kusaka kura. Maneno yamekuwa mengi zaidi kuliko utendaji. Kila kukicha mipango inapangwa na kupanguliwa kana kwamba hatuna wasomi na viongozi.
Wakulima wananyonywa kila uchwao huku kasi ya kutatua matatizo yao haionekani kulingana na matatizo yanayowakabili. Mara stakabadhi ghalani, mara mbolea na pembejeo za ruzuku.
Mara utasikia utaratibu wa kununua mbolea kwa pamoja umefutwa, mara umerejeshwa, kule utasikia agizo la kuzuia kuuza mahindi nje ya nchi huku utasikia zuio limeondolewa. Mara utasikia mwenye mazao chini ya tani moja asilipe ushuru mara utasikia walipe.
Yaani kilimo kimegeuzwa siasa inayofanyika shaghala baghala. Mabilioni ya fedha za wahisani na walalahoi zinapotea kwenye programu zisizo endelevu.
Leo hii tunakukumbuka Nyerere kwa kuweka picha zako kila sehemu, kuandika hotuba, kuandaa matamasha na mashindano ya kila aina ambayo ukiyatazama kwa undani ni kutafuta na kutafuna fedha iwe za umma au za watu binafsi.
Tunarudia kisikiliza na kuangalia hotuba zako kila kukicha, zimebeba matumaini ya kila Mtanzania kwamba mtoto wake angeweza kusoma, mgonjwa kupata vipimo na matibabu ya uhakika, mfanyakazi na mkulima angenufaika na shughuli anayoifanya. Tuulizane mambo yanakwenda kama tulivyotarajia?
Tukimaliza kuangalia na kusikiliza hotuba za Nyerere tunachukua hatua gani? Kuna mwenye kupiga kelele anapoona au kusikia haki ya mwingine inasiginwa, kuna mwenye ubavu wa kukemea pale Mtanzania anapopatiwa huduma isiyostahili?
Je tunapowaona wazee wanateseka kusaka pensheni au matibabu tunathubutu kufungua midomo yetu au ndiyo tumekosa ujasiri wa kukabili watawala?
Tunawezaje kujinasibu tunamuenzi Mwalimu Nyerere wakati tumejawa na chuki tukifurahia na kuwaombea mabaya wenzetu iwe wawe kwenye taasisi za umma au binafsi?
Mwalimu Nyerere ulitusihi sana tujitegemee, ukadiriki hata kutuambia uhuru bila kujitegemea ni bure. Leo hii tunalilia misaada na kutoa maneno ya kejeli kwa wanaotuminyima. Rasilimali zetu zinanufaisha wachache huku wengi wakiogelea kwenye lindi la umasikini.
Tukimaliza kukumbuka Mwalimu Nyerere tunaendelea na maisha yetu kama kawaida tena mengine yakipingana kabisa na kile ulichotuasa.
Naamini kumbukumbu nzuri ingepaswa kila mmoja wetu kuchukia rushwa kwa vitendo, kukataa uonevu, ubaguzi iwe wa kidini, kiitikadi na kimaeneo. Tungejivunia zaidi kama tungejitegemea na kupunguza pengo kati ya walionacho na wasionacho. Watawala na watawaliwa.
Kufanya kumbukumbu ya Nyerere bila ya kufuata mazuri aliyoyafanya ni kutomtendea haki. Nyerere hakuwa malaika kwa kuwa kuna mabaya aliyoyafanya hayo tunachane nayo.
Nakumbuka katika moja ya hotuba zake alishakiri uongozi wake ulifanya mazuri na mabaya, alishatuonya tuache utamaduni wa kuchukua mabaya na kuyafanya hoja za msingi.
Mwisho.