KWA muda mrefu nimeaminishwa nisiwaamini moja kwa moja wanasiasa, niliambiwa mwanasiasa akinisalimia ‘habari za asubuhi’ nisijibu haraka bali nihakikishe kwanza kama ni kweli asubuhi.Anaandika mwandishi wetu, Salehe Mohamed … (endelea).
Niliambiwa nihakikishe kwanza kama kweli ni asubuhi kwakuwa naweza kuitikia salamu isiyoendana na wakati. Nami napenda nitoe au niitikie salamu inayoendana na wakati.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Idara ya Oganaizesheni, Paul Chacha. Wamenifanya nikumbuke tahadhari niliyopewa dhidi ya wanasiasa.
Chacha ameutangazia hadharani kuwa vyombo vyote vya dola, mawaziri na viongozi wa serikali na taasisi zake ni mali halali ya CCM. Kwa wanaojua Katiba walisema hakuwa sahihi.
Prof. Kabudi anatuambia kuwa “Vyombo wa dola ni vyetu sote, ninavyosema vyombo vyetu ni vyombo vya Taifa, vyombo hivi ni vya Watanzania wote, vyombo hivi vya ulinzi na usalama ni vya Watanzania wote, ni vyombo vyetu sote.”
Sina uhakika nani yuko sahihi ila ninachofahamu hawa wawili wapo kwenye chama kimoja, wote ni viongozi wa juu.Wote wanaoongozwa na kuzingatia Katiba ya Tanzania na CCM.
Sijajua kama kuna mwanya wa mmoja wao kusema au kufanya tofauti na miongozo iliyowekwa. Sina hakika nani ataaminika zaidi mbele ya jamii kulingana na mazingira tuliyonayo.
Chacha anatuambia CCM ndicho kinateua mawaziri, mkuu wa majeshi, mkuu wa jeshi la polisi, magereza, usalama wa taifa, wakurugenzi wa halimashauri, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya. Hili si la kubishaniwa.
Kama vyombo vya dola ni mali yetu sote kwa nini wakosoaji wa serikali ndiyo wanaopigana vikumbo kwenye magereza, vituo vya polisi na mahakamani kwa tuhuma ambazo hata asiyejua sheria anaziona zina chembechembe za kudhoofishana kisiasa?
Moyo wangu unatamani kukubaliana na Prof. Kabudi lakini akili yangu inanikatalia kwa kunipa maswali ya hatua gani zilichukuliwa kwa wana-CCM waliowaonya Polisi walifuatilie wakiwapoteza wenzao wa upinzani?
Inaniuliza hatua zipi za kisheria zilichukuliwa kwa yule aliyetangaza kufanya kazi za porini ‘kuwanyoa’ wapinzani ili kuwapa ushindi wagombea wa CCM.
Katika mazingira haya, wananchi wamuamini Paul Chacha au Prof. Kabudi ambaye tuna historian aye ndefu tu katika suala la makinikia na dawa za Uviko-19 kutoka Madagascar enzi za utawala wa Rais John Magufuli.

Chacha na Kabudi wanaongea lugha gongana lakini kiuhalisia wote ni wanufaika wa ‘CCM kumiliki vyombo vya dola.’ Inawezekana Kabudi kajitokeza ili kusafisha hali ya hewa iliyochafuliwa na mwenzake anayelaumiwa kwa kusema ukweli mchungu.
Si ajabu wameshamfunda Chacha kwa kumuambia ‘ukila na kipofu usimshike mkono’ ndiyo maana Prof. Kabudi kajitokeza kuweka mambo sawa. Kwa kizazi cha sasa sina hakika kama ataeleweka.
Serikali na vyombo vyake vinapaswa kuwa ni mali ya wananchi si mali ya CCM au chama chochote kitakachoingia madarakani. Mwanasiasa anayejigamba vyombo hivyo ni mali ya chama alichomo huyo amezidiwa na utamu wa madaraka.
Katiba ya Tanzania imetoa ulinzi maalumu dhidi ya kuchanganya vyombo vya ulinzi na siasa. Ibara ya 147(3) inakataza mfanyakazi wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwa mwanachama wa chama cha siasa (isipokuwa haki yake ya kupiga kura).
Nina hakika Chacha amesoma lbara ya 8 ya Katiba inayoweka msingi thabiti kwamba mamlaka na nguvu zote za Serikali zinatokana na wananchi na Serikali inawajibika kwa wananchi.

Sasa anapotueleza kuwa vyombo vya dola na viongozi wa Serikali ni mali yao (CCM), si ndiyo anathibitisha yale madai kuwa hata zile taarifa za kitelijensia za Jeshi la Polisi wanazozitumia kuzuia mikutano ya hadhara, maandamano ya amani ya wapinzani ni lengo la kukibeba chama tawala na si kwa sababu za kiusalama.
Kama CCM wanamiliki vyombo vya dola watashindwa vipi kuvitumia kudhoofisha wapinzani wao katika maeneo ambayo wanaona wana ushawishi mkubwa?
Chacha na Prof. Kabudi wamechochea madai ya Katiba mpya bila kutambua. Mamlaka ya kuteua na kutengua aliyonayo Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Tanzania ndiyo yanayowafanya makada wa chama hicho tawala wajione wanamiliki vyombo vya dola na viongozi wake.
Tutengeneze mifumo ya wakuu wa taasisi za umma na vyombo vya dola kupatikana kwa kuomba kazi hizo na viwepo vyombo vya kuwachuja, kuwahoji na hatimaye kumpitisha anayefaa. Tupunguze utaratibu wa kuteuana.
Katika mazingira tuliyonayo ni nadra kwa anayeteuliwa kwenda kinyume na matakwa ya aliyemteua. Ni vema tukatengeneza Katiba yetu hivi sasa kuliko kusubiri mambo yaharibike ndipo tushtuke.
Chacha anaamini CCM ni mmiliki wa vyombo vya dola hivyo anaweza kuvitumia kadri anavyoona inafaa, Prof. Kabudi anatuambia ni mali yetu sote. Jakaya Kikwete alisema “akili za kuambiwa changanya na zako.”
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ni mali ya CCM. Hata viongozi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni mali ya CCM. Nani anabisha?
Mwisho.