CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetuhumu uongozi wa Gereza Kuu la Ukonga jijini Dar es Salaam kumzuia Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Edward Mapunda, kumuona Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama hicho.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Lissu yuko mahabusu kwenye gereza hilo akikabiliwa na kesi ya uhaini iliyosikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam mbele ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.
Shauri hilo liko katika hatua za mwisho ambapo mahakama inasubiriwa kutoa hukumu tarehe 6 Novemba mwaka huu.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano ya chama hicho Brenda Rupia ilieleza kuwa Askofu Mapunda jana tarehe 11 Oktoba alifika kwenye gereza hilo kwa lengo la kutaka kumjulia hali na kufanya naye ibada.
Taarifa ya Rupia imeeleza kuwa licha ya Askofu Mapunda kuambiwa asubiri ili amuone Lissu lakini hakupata nafasi ya kuonana naye licha ya kukaa kwa takriban saa nne.
“Alijulishwa kuwa hawezi kumuona bila kibali cha Kamishna wa magereza”.
Chadema imetoa wito kwa viongozi wengine wa dini kutafakari hatua hiyo .
Jitihada za MwanaHALISI digital, kuupata uongozi wa gereza hilo kuzungumzia tuhuma hizo zimegonga mwamba kutokana na simu zao kuita bila majibu.
Mwisho.
