RAIS wa Kenya, William Ruto, ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu waliopoteza maisha katika ajali ya helikopta nchini Zimbabwe, akiwemo mfanyabiashara maarufu Wicknell Chivayo, mke wake Lucy Muteke na abiria wengine sita.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Ruto ameandika katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii leo 1 Oktoba 2026 akisema amesikitishwa na kifo cha ghafla cha rafiki yake Chivayo, pamoja na mke wake na watu wengine waliokufa katika ajali hiyo.
“Nimesikitishwa sana na kifo cha kusikitisha cha rafiki yangu, Wicknell Chivayo, pamoja na mke wake, Lucy Muteke, na watu wengine waliopoteza maisha katika ajali ya helikopta nchini Zimbabwe. Kuondoka kwao ghafla ni pigo kubwa kwa familia zao, marafiki na wote waliowafahamu,” ameandika.
Rais Ruto amesema Chivayo alikuwa rafiki yake wa karibu ambaye upendo na uchangamfu wake uliwagusa watu wengi.
“Wicknell alikuwa rafiki yangu mpendwa ambaye uchangamfu wake uliwagusa watu wengi. Nitakumbuka urafiki wake, nguvu zake na imani yake kubwa kuhusu uwezekano na fursa zilizopo katika bara letu,” amesema.
Ametoa pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa, wananchi wa Zimbabwe na wote walioomboleza kutokana na msiba huo.