RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amekosoa madai yanayohusisha vyombo vya dola na chama cha siasa, akisisitiza kuwa taasisi za ulinzi na usalama zinapaswa kuwajibika kwa Katiba, sheria na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Katika andiko lake lenye kichwa “Dhihaka na Matusi kwa Katiba,” Mwabukusi amesema vyombo vya dola hutumia mamlaka ya umma kwa niaba ya Jamhuri na wananchi, hivyo havipaswi kuchukuliwa kuwa mali ya chama chochote cha siasa.
Ameeleza kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) vina wajibu wa kulinda taifa na wananchi wote bila kujali itikadi au chama wanachokifuata. Amesisitiza kuwa taasisi hizo zinapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba na sheria.
Mwabukusi amesema chama cha siasa kinaweza kushinda au kushindwa uchaguzi na Serikali inaweza kubadilika, lakini vyombo vya dola vinaendelea kuwa taasisi za Jamhuri na wananchi.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Mwabukusi amesema madai ya upendeleo katika utekelezaji wa majukumu ya vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na madai ya ukiukaji wa haki, yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kufanyiwa uchunguzi huru.
Pia ametoa wito wa uwazi na uchunguzi kuhusu madai ya utekaji na matumizi ya vyombo vya dola kwa misingi ya kisiasa, akisema wananchi wanahitaji kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo.
Mwabukusi amesisitiza kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwa waaminifu kwa Katiba, sheria na Jamhuri badala ya chama chochote cha siasa. Amehitimisha kwa kueleza kuwa juhudi za kujenga taifa haziwezi kuwa na matokeo bila ukweli, haki na uwajibikaji.