MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini anaendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho (final submissions), akijielekeza katika hoja za kisheria na kuhoji kama maneno anayodaiwa kusema yanaweza kisheria kuunda kosa linalomkabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza jana tarehe 23 Septemba 2026, mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Lissu alianza kuwasilisha hoja zake za utetezi, ambapo kufikia saa 11 jioni alikuwa ameeleza mahakama mambo matatu kati ya tisa ambayo anaona ni muhimu yakaamuliwa kutokana na mkanganyiko wake.
Katika hoja zake, Lissu alisisitiza kuwa hakatai kusema maneno yanayotajwa na upande wa mashtaka, lakini hoja yake ni kama maneno hayo yanatimiza masharti yote yanayohitajika kisheria kuthibitisha kosa hilo.
Alisema, yeye hakuitisha mkutano wake na watia nia uliofanyika 3 April 2025, pia si yeye aliyeitisha waandishi wa habari na kuwa kesi hiyo ya uhaini inayomkabili haikufunguliwa kwa mujibu wa sheria akifafanua mkanganyiko huo ambao ataendelea kuufafanua leo.
Alisema, “Kuchochea umma” si kosa lililotajwa kwenye sheria,” na hivyo kuitaka Mahakama kuzingatia sheria wakati wa kutoa uamuzi wake.
Moja ya hoja kuu za Lissu ilikuwa kuhusu lugha iliyotumika kwenye hati ya mashtaka. Alisema kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu kinachotumika katika kesi hiyo kinahusu kutishia Serikali kupitia kuchochea mtu au kikundi cha watu, wakati hati ya mashtaka inatumia maneno “kuchochea umma.”
Kwa mtazamo wake, tofauti hiyo ni muhimu kwa sababu mahakama haiwezi kutengeneza kosa ambalo halijaainishwa na sheria.
Aidha, mwanasiasa huyo mashuhuri nchini, alihoji shitaka la kutishia “Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” akitaka kujua ni sehemu gani ya Serikali inayodaiwa kutishiwa na kauli zake.
Alipinga ushahidi unaohusisha maandalizi ya mkutano wa chama chake wa wa 3 Aprili 2025. Alisema, hakuuitisha wala kuuandaa mkutano huo, bali alikuwa mmoja wa watu walioalikwa. Kwa mujibu wa hoja zake, maandalizi ya mkutano yalifanywa na Sekretarieti ya chama hicho.
Hivyo, alitaka mahakama izingatie ushahidi uliotolewa kuhusu nani aliyeandaa mkutano huo na nafasi yake binafsi katika maandalizi hayo.
Lissu pia alihoji ushahidi kuhusu kualika waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo, akipinga kuhusika na kualika, lakini pia kuchapisha maudhui ya video ya mkutano huo mtandaoni kupitia Jambo TV.
Wakati wa maswali yake kwa shahidi mkuu wa upelelezi, Lissu alihoji kama yeye ni mfanyakazi, mtangazaji au mpiga picha wa Jambo TV, na kama alikuwa na nywila ya kuingia kwenye mfumo wa chombo hicho.
Lissu pia alisisitiza kwamba kukiri kusema maneno yanayodaiwa hakumaanishi amekiri kosa la uhaini.
“Maneno pekee hayatoshi kuthibitisha uhaini”
Kwa mujibu wa hoja yake, mahakama inapaswa kuangalia maana ya maneno hayo, mazingira yalipotolewa na ushahidi mwingine wa kesi, kisha kuamua kama vipengele vya kosa linalomkabili vimethibitishwa.
Upande wa mashtaka, kwa upande mwingine, unasema maneno hayo na mazingira yalipotolewa yanaonyesha dhamira ya kutishia Serikali na kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025.
Katika kuunga mkono hoja zake kuhusu namna sheria inavyopaswa kutumika katika kesi za jinai, Lissu pia alirejea kesi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.
Lissu alitumia mfano huo katika kueleza hoja zake kuhusu namna mahakama inavyopaswa kufuata sheria na ushahidi uliowasilishwa badala ya kuunda kosa ambalo halijaainishwa kisheria.
Kingine Lissu alichosema jana ni kuhusu uamuzi katika kesi yake kwamba hautamhusu yeye pekee, bali unaweza kuweka msingi wa kisheria ambao mahakama zinaweza kuufuata katika miaka ijayo.
Alisema, kesi yake ni tofauti na kesi mbili za uhaini alizotaja za Grey Likungu Mataka na wenzake ya mwaka 1970, na Hatibu Gandhi na wenzake ya mwaka 1983, ambazo alisema zilihusu madai ya kujaribu kuipindua Serikali au kumuua Rais.
Kwa mujibu wa Lissu, kesi yake chini ya kifungu cha 39(2)(d) inahusu madai ya kutishia Serikali kwa kuchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025.
“Leo nimezungumzia sheria. Naomba tuendelee kesho. Nataka kuzungumzia ushahidi.”Anasema Lissu akihitimisha hoja zake jana.