RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi amesema kuwa taifa la Zanzibar limefikia maridhia bila kupatanishwa na shirika au watu kutoka nje ya nchi.Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Dk. Mwinyi ameyasema haya leo tarehe 22 Septemba 2026, wakati wa uapisho wa Makamo wa Kanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ‘OMO’,.
Mwinyi ameeleza kuwa hatua ya Kumwapisha OMO ni matokeo ya maridhiano hayo.
“Hatua hii ya kumuapisha Makamo wa Kwanza wa Rais ni matukio ya maridhiano kati ya Chama Cha Mapinduzi na chama cha ACT-Wazalendo yaliyopelekea kusainiwa kwa tamko la pamoja la maridhiano tarehe 9 Julai 2026 katika viwanja hivi vya Ikulu.
Cha kujivunia kwamba maridhiano haya yamefikiwa bila kuhusisha mtu au taasisi yoyote ya nje ya nchi kwa hakika huu ushahidi wa dhamira ya dhati tulionayo ya kuweka mbele maslahi ya taifa,” amesema Dk. Mwinyi.
Amesema kuwa hatua hiyo ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na uwezo binafsi wa kutafuta suluhu kwa masuala ya taifa hilo kwa mazungumzo.
Tangu kumaliza kwa uchaguzi mkuu wa tarehe 28/29 Oktoba mwaka jana nchi hiyo haikuwa na serikali ya umoja wa kitaifa kama yalivyo matakwa ya Katiba ya Zanzibar ibara ya 9(3) baada ya marekebisho ya mwaka 2010.
Kwamba chama cha pili kwenye uchaguzi mkuu kitaunda serikali kwa kuwa na Makamo wa Kwanza wa Rais na kushika baadhi ya wizara.
Chama kikuu cha Upinzani visiwani humo (ACT) ambacho mwenyekiti wake ni OMO, kiligoma kuingia kwenye serikali hiyo kwa madai ya kuwa uchaguzi ulikuwa una hila na ulichafuliwa kwa makusudi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza serikali hiyo.