WAJUMBE wawili wateule wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui na Omar Said Shaaban, walioteuliwa mapema wiki hii, wameapishwa rasmi barazani. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Mbele ya Spika wa Baraza hilo, Zubeir Ali Maulid, wajumbe hao kutoka Chama cha ACT Wazalendo, waliingia kwa shangwe barazani, Mazrui akianza kushika kitabu kitukufu cha Kuran, na kula kiapo cha uaminifu na ahadi ya kuilinda Katiba ya Zanzibar.
Mazrui ambaye ni Naibu Katibu mstaafu wa chama, alifuatiwa na Omar ambaye ameteuliwa mwakilishi huku kwenye chama akiwa Mwanasheria Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu.
Wakiwa wameketi kwenye viti barazani, mara baada ya kuapishwa, alikuwa Omar aliyepata nafasi ya kuruhusiwa kuzungumza pale alipoinuka na kuuliza swali la msingi kwa niaba ya Mwakilishi wa Viti Maalum kupitia ACT Wazalendo, Jabu Makame Juma, swali lililoihusu Wizara ya Kilimo na Mifugo.
Isitoshe, baada ya swali la msingi kujibiwa, Omar alisimama na kuuliza swali la nyongeza akitaka kujua ni mmiliki wa maghala ya kuhifadhia bidhaa yaliyo chini ya wizara hiyo.
Wawakilishi Mazrui na Omar, waliteuliwa juzi Jumatatu, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika uteuzi alioufanya siku chache baada ya kukamilika kwa mazungumzo ya kupata muafaka wa kisiasa kati ya chama hicho na Chama Cha Mapinduzi [CCM].
Wote hao walikuwa wajumbe wa baraza hilo kupitia uteuzi kama huo baada ya uchaguzi wa 2020. Wakateuliwa kushika uwaziri – Mazrui akikabidhiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakati Omar akipewa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.
Kwenye uchaguzi uliopita 2025, Mazrui aligombea kiti cha jimbo la Mwera huku Omar akiwania jimbo la Pangawe.