KAMATI ya Majadiliano yenye jukumu la kuchambua makubaliano yaliyofikiwa na vyama vya CCM na ACT Wazalendo imezinduliwa leo katika hafla ilofanyika Ikulu mjini Zanzibar. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Chama Cha Mapinduzi [CCM] na ACT Wazalendo vimechangia wajumbe wa Kamati hiyo ya watu kumi ikiongozwa na wenyeviti wenza wawili.
Kamati hiyo iliyoteuliwa jana na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi na taarifa yake kutolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mansura Mossi Kassim, inaongozwa na Abdi Mahmoud Abdi na Omar Ali Shehe ambao ni manaibu katibu wakuu kwenye vyama vyao – Abdi akiwa CCM na Omar ACT Wazalendo.
Akihutubia hadhara hiyo iliyojumuisha viongozi waandamizi wa vyama hivyo, Dk. Mwinyi alisema kamati imepewa muda wa miezi mitano kufanya kazi waliyopangiwa na kwamba inawezekana muda kuongezwa.
Lakini ameeleza kuwa kukitokea tatizo kwa namna yoyote ile katika utekelezaji wake, Kamati inayo fursa ya kutaka ushauri kwake yeye na pia kwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman.
“Sisi wawili tupo kuwasaidia kusonga mbele. Mmeteuliwa kwa sababu mnao uwezo. Tunawaamini na wananchi wana matarajio makubwa nanyi. Mufanye kazi kwa kuifikiria nchi yetu. Mtafute suluhisho badala ya kuendeleza migogoro,” alisema.
Akitoa nasaha kabla ya uzinduzi wa Kamati hiyo, Othman Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Rais Zanzibar alisema jukumu lililo mbele ya kamati, si la kisiasa bali zaidi, ni la kuijenga nchi ifike kwenye matumaini ya wananchi.
“Mjue mnalo jukumu la kuisaidia nchi kudumisha amani na utulivu ambavyo ndio huleta uwekezaji unaochagiza kukua kwa uchumi wa Zanzibar ambao kwa asili yake ni uchumi wa huduma.
“Hakuna atakayekuja kuwekeza pakiwa na siasa chafu na mivutano. Mjue uadilifu na nidhamu vinahitajika katika kutekeleza jukumu mlilopewa. Kila nchi ina nyakati zake za kiza kabla ya mafanikio na Zanzibar imepita huko. Lakini sasa inahitaji historia yake mpya. Historia inayoakisi asili yake ya kuwa nchi yenye itukufu mkubwa katika mambo mbalimbali,” alisema.
“Tafadhalini nendeni mkafanye kazi kwa uadilifu na imani kubwa ili kuiletea nchi kile inachokistahili,” alisisitiza.
Mbali na wenyeviti wenza Abdi na Omar, wajumbe wengine wa Kamati ni: Kutoka CCM – Dk. Khalid Salum Mohamed, Najma Murtaza Giga, Masoud Ali Mohamed na Mgeni Hassan Juma.
ACT Wazalendo: Omar Said Shaaban, Fatma Abdulhabib Fereji, Said Ali Mbarouk na Mohamed Nur Mohamed.
Makatibu wa Kamati: Mwalim Ali Mwalim na Seif Khamis Mohamed wakati wafuatao wameteuliwa kuunda Sekretarieti ya Kamati:
Hamid Saleh Mhina, Mohamed Yusuf, Ali Salum Khamis na Abdalla Mussa Hijja.