USHAHIDI MAUAJI YA SHEIKH JABIR HAIDAHATIMAYE kesi ya mauaji ya Sheikh Jabir Haidar Jabir leo imeanza rasmi kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu Zanzibar mbele ya Jaji Khadija Shamte. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo inayowakabili watu watatu wanaotuhumiwa kuua kwa makusudi, umeleta mashahidi wawili na wote walitoa ushahidi ukakamilika.
Mashahidi hao ni Juma Suleiman Khamis (68), ambaye ni Sheha wa Shehia ya Kizimbani, na Kassim Haidar Jabir ambaye ni kaka wa marehemu. Waliongozwa shahidi na Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Khamis Othman.
Akitoa ushahidi mahkamani, Shahidi wa kwanza ambaye ni Sheha wa Shehia ya Kizimbani, Wilaya ya Magharibi A, Unguja, aliieleza mahkama kuwa siku ya tarehe 27 Mei 2025, alipigiwa simu kiasi cha Saa 3:15 usiku na askari wa JKU na kujulishwa kuwa kuna maiti imekutwa eneo lake la utawala.
Shahidi: Nikaenda eneo la tukio na kukuta maiti pembeni mwa barabara inayokwenda Bumbwisudi.
“Hawa askari wa JKU walionipigia simu kunipa taarifa ni walinzi wa visima vya maji vilivyopo karibu na eneo ambako mwili wa marehemu ulikutwa.”
“Nilipofika nilishuhudia mwili ulioonesha umetupwa sehemu ile ambayo ni mabonde ya mpunga, kuutizama mwili nikabaini ni mtu ambaye ameshakufa. Nikapiga simu Polisi na ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kutoa taarifa kwa ajili ya hatua zinazofuata.”
Shahidi alieleza mazingira ya sehemu ambayo mwili ulikutwa ikionesha mwili huo umetupwa tu pale lakini tukio la kuuliwa kama lililofanyika sehemu nyengine.
Aliieleza mahkama kuwa hali ya mwili alikuta umelala, mtu alikuwa amevaa viatu vya yeboyebo, kanzu rangi buluu na vespa iliyokuwa kando ya ulipokutwa mwili.
Hakuukagua kwa mikono maana alieleza wapo wahusika wa kufanya uchunguzi na kwamba kazi yake yeye Sheha ni kuwajulisha tu.
Sheha aliendelea: Polisi walipofika na kushuhudia mwili walipiga picha na kuuchukua mwili, wakaupakia kwenye gari na kuondoka nao.
Mwendesha Mashtaka alimuuliza Sheha Juma alijuaje kama mtu huyo alikuwa amekufa wakati yeye si mtaalam.
Alijibu kwa utu uzima alio, mwenye akili timamu, anajua sura na mazingira ya mtu ambaye amekufa.
Hoja hiyo iliibuka tena Shahidi huyo alipohojiwa na wakili wa upande wa utetezi Leonard. Alimuuliza alijuaje kama mtu amekufa, kwani yeye ni mthibitishaji kifo? Shahidi: “Najua mimi si mthibitishaji wa mtu kufa, hayo watayaeleza wahusika lakini nikimtizama mtu ninajua kama amekufa.”
Shahidi huyo pia alihojiwa na Wazee wa Mahkama kama aliukuta wapi mwili. Alijibu aliukuta umetupwa pembeni mwa barabara eneo la Kizimbani njia ya kuelekea Bumbwisudi.
Shahidi alipoulizwa aliukuta mwili katika mazingira gani, alijibu haukuonesha mtu alipigwa panga au silaha kama hiyo. Kuhusu muda khasa ambao Polisi waliwasili eneo la tukio, alijibu “kunako Saa nne hivi usiku.”
Shahidi wa pili ni Kassim Haidar Jabir ambaye ni Mwanasheria na kaka wa marehemu, aliiambia Mahkama kuwa alipigiwa simu usiku ulioanza kuingia tarehe 28 Mei na kujulishwa kuwa afike mochwari ili kuutambua mwili uliokuwa umehifadhiwa kwenye Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Unguja.
Shahidi: Nilikimbilia huko na kuonana na msimamizi wa mochwari (Chumba cha kuhifadhia maiti) nikamtambua maiti ni ya Jabir Haidar Jabir ambaye ni mdogo wangu wa tano kwa kuzaliwa, baba mmoja na mama mmoja.
Baada ya kumtambua alitakiwa kusuburi mwili ufanyiwe uchunguzi. Alipoulizwa alikuta mwili uko katika hali gani, alijibu “Mwili umeanza kuvimba, mikono ikiwa imekunjika (anaonesha kwenye tumbo), na eneo la viganja kuna alama ya kamba ikiashiria alifungwa. Shingoni kulikuwa na alama ya kamba na mabaki ya pamba kama iliwekwa ikaondolewa.”
Pale alifika Mkemi akataka ruhusa kwetu waupasue mwili ili kuchunguza zaidi kilichomsibu. Nilikubali kuruhusu na wakafanya uchunguzi wao kuanzia saa 6 mpaka 7 hivi usiku hadi ulipokamilika Saa 10 alfajiri.
Baada ya uchunguzi waliruhusiwa kuchukua mwili kwa ajili ya mazishi. Alipoulizwa walimzika wapi? Kassim alijibu kwenye Makaburi ya Mwanakwerekwe.
Wakili wa utetezi alimhoji Shahidi huyo akimuuliza kaka alivyoukuta mwili ilikuwa maiti amefungwa kamba? Shahidi: Hapana, nilikuta alama ya kamba mikononi, mwili umevimba mshipa wa shingo [anaonesha) umetokeza na mikono imekakamaa hapa kifuani (anaonesha). Akaulizwa hivi mpaka sasa hamjui nyinyi amekufaje na mtajuaje? Shahidi: Hatujui maana mimi sijaisoma ripoti ya daktari.
Watuhumiwa watatu kwenye kesi hiyo ni Salum Manja Ame (23) Mkaazi wa Darajabovu, Idrisa Kijazi Kassim (41) Mkaazi wa Tomondo na Ali Mohammed Ali (30) anayeishi Kijichi.
Wanatuhumiwa kutenda kosa kinyume na Sheria ya Adhabu Namb 6 ya mwaka 2018 kifungu 179 na 180.
Watuhumiwa Ali Machano Haji (52), Zahor Khamis Ali (54) na Mohammed Hassan Jongo (38) ambao awali walikamatwa kwa tuhuma za mauaji ya kukusudia, waliachiwa katika hatua za awali za kesi hiyo.
Kesi hiyo imeakhirishwa mpaka tarehe mosi Oktoba 2026. Mwendesha Mashtaka Khamis Othman ameahidi siku hiyo kuleta mashahidi wengine watatu.