MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutumia mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuondoa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Wakili Tundu Lissu.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
THRDC imesema hatua hiyo inaweza kufungua njia ya maridhiano ya kitaifa na kusaidia kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya nchini.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam 20 Agosti 2026 kupitia Taarifa ya Awali ya Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Kesi hiyo, iliyowasilishwa na Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa.
Taarifa hiyo imetathmini mwenendo wa shauri hilo pamoja na hali ya Lissu akiwa kizuizini tangu alipokamatwa 9 Aprili 2025.
THRDC imeeleza kuwa kuendelea kwa shauri hilo mahakamani kunakwamisha jitihada za maboresho ya kisheria, kuzuia nafasi ya maridhiano ya kisiasa na kuchelewesha mchakato wa Katiba Mpya.
Mtandao huo umeitaka Serikali kutumia mifumo halali iliyopo, ikiwemo mamlaka ya DPP inapofaa na kwa mujibu wa sheria, ili kutafuta suluhisho linalozingatia haki, umoja wa kitaifa na mshikamano wa kijamii.
THRDC pia imetaja hatua zilizowahi kuchukuliwa katika shauri lililomhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ikisema uzoefu huo unaweza kuzingatiwa katika suala la Lissu.
Aidha ripoti hiyo, iliyokusanywa na timu ya wataalamu wa sheria na habari iliyoongozwa na Wakili Paul Kisabo, imebainisha madai kadhaa kuhusu changamoto za haki za binadamu katika kipindi ambacho Lissu amekuwa kizuizini.
Bila kuingilia uhuru na maamuzi ya Mahakama, THRDC imelishauri Bunge kurekebisha Kifungu cha 151(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Kwa mujibu wa mtandao huo, marekebisho hayo yanapaswa kurejesha mamlaka ya Mahakama kufanya tathmini ya maombi ya dhamana kwa kuzingatia mazingira ya kila kesi.
THRDC imesisitiza kuwa matumizi ya mifumo halali ya kisheria yanaweza kusaidia kuweka mazingira ya maridhiano ya kitaifa, kuimarisha umoja na mshikamano wa kijamii, pamoja na kufungua njia ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya nchini.