CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepinga uamuzi wa Serikali kupitia Idara ya Habari Maelezo wa kusitisha leseni ya gazeti la MwanaHALISI kwa kipindi cha miezi sita kuanzia 19 Aprili 2026.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Katika taarifa iliyotolewa leo 20 Agosti 2026, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, amesema chama hicho kinaitaka Idara ya Habari Maelezo kuhakikisha kuwa hatua zote zinazochukuliwa dhidi ya vyombo vya habari zinaendana na misingi ya haki, uwiano, usawa na adhabu inayolingana na kosa.
Rupia amesema mamlaka hazipaswi kutumika kama chombo cha kuzima sauti zinazokosoa Serikali au zile zinazoibua masuala yenye maslahi kwa umma.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Chadema imesema hatua dhidi ya MwanaHALISI ni sehemu ya mwenendo unaotia wasiwasi kuhusu matumizi ya mamlaka za Serikali katika kudhibiti na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uhuru wa kujieleza nchini.
Aidha, chama hicho kimetoa wito kwa wanaharakati wa haki za binadamu, watetezi wa demokrasia, vyama vya siasa, vilabu vya waandishi wa habari, Jukwaa la Wahariri na wadau wengine wa sekta ya habari kupaza sauti na kusimama pamoja katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza nchini.