MKOA wa Dar es Salaam umeongoza kwa matumizi na idadi ya vifaa vya kujipima maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) vilivyosambazwa nchini mwaka 2025, baada ya kupokea vifaa 330,351.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) ya mwaka 2025, jumla ya vifaa 2,494,398 vya kujipima VVU vilisambazwa nchini katika kipindi hicho.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa Dar es Salaam ilipokea vifaa 330,351, sawa na takribani asilimia 13 ya vifaa vyote vilivyosambazwa nchini.
Mkoa huo ulifuatiwa na Mbeya uliopokea vifaa 221,963, Tabora 200,784, Pwani 188,351 na Tanga 179,533.
Huduma ya kujipima VVU, inayojulikana kama HIV self-testing, inalenga kuongeza wigo wa upimaji kwa kuwapa wananchi fursa ya kujua hali zao kiafya kwa faragha, urahisi na muda unaowafaa.
Huduma hiyo imekuwa ikilenga zaidi kuwafikia makundi ambayo yanaweza kukumbana na changamoto za kufika katika vituo vya afya, wakiwemo wanaume na vijana.
NASHCoP, ambayo ipo chini ya Wizara ya Afya, imeeleza kuwa tafiti zimeonesha matumizi ya vifaa vya kujipima VVU kuwa makubwa zaidi katika maeneo ya mijini ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.
Ongezeko la matumizi ya vifaa hivyo linaonekana kuwa sehemu ya juhudi za kupanua huduma za upimaji wa VVU na kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wale wanaopendelea kufanya upimaji kwa faragha.