MAMLAKA za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo zimeripoti ongezeko la vifo vinavyohusishwa na mlipuko wa Ebola aina ya Bundibugyo ya ugonjwa wa Ebola ambapo idadi imefikia 506. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Kufikia tarehe 4 Julai 2026, jumla ya visa 1,561 vilivyothibitishwa vimeripotiwa tangu mlipuko huo kutangazwa Mei 15 na kwa sasa wagonjwa 628 wamelazwa au wametengwa katika vituo vya afya.
Mkoa wa Ituri unaendelea kuwa kitovu cha maambukizi, ukichangia zaidi ya asilimia 90 ya visa vyote. Unafuatiwa na North Kivu na South Kivu.
Maeneo yaliyoathirika yanakadiriwa kuwa na wakazi takriban milioni 15. Kati ya hayo, kuna maeneo 36 ya afya yaliyo katika hatari kubwa kutokana na uhamaji mkubwa wa watu unaosababishwa na migogoro na shughuli za uchimbaji madini.
Wafanyakazi wa afya 96 wameambukizwa, huku 19 wakifariki, na watu 10,079 wameorodheshwa kufuatiliwa baada ya kugusana na wagonjwa.