Said Issa Mohamed
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, amemtaka Said Issa Mohammed, aliyekuwa mwanachama wa chama hicho, kufuata taratibu za kikatiba ili kupata suluhu ya uanachama wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Said Issa Mohammed, alifutwa unachama wake na Kamati Tendaji ya Kanda ya Pemba, kufuatia tuhuma za usaliti, baada ya kukifikisha mahakamani chama chake.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Jumatatu, tarehe 6 Julai 2026, akiwa nje ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Mnyika amesema, Said ameenda kukishtaki Chadema, Msajili wa Vyama vya Siasa badala ya kukata rufaa ndani ya chama.
Amesema, Ofisi ya Msajili imekiandikia chama chake barua ikikitaka kijieleze, kwanini kimemfuta uanachama Issa, jambo ambalo wamesema, mlalamikaji anapaswa kufuata taratibu za rufaa za Chadema, ili kulinda uanachama wake.
Mnyika alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya kutoka mahakamani, kusikiliza shauri lililofunguliwa na Issa na mwenzake mmoja, kutaka kuwapo mgawanyo sawa wa mali za chama hicho.
Chadema imeweka pingamizi juu ya madai hayo. Ametoa siku 10 kwa chama hicho kueleza kiini cha pingamizi lake, huku walalamikaji wakipewa hadi tarehe 3 Agosti, kujibu hoja za Katibu Mkuu wa Chadema na bodi ya wadhamini ya chama hicho.
Said Issa na mwenzake, wamefungua kesi dhidi ya Chadema, wakitaka mahakama hiyo, kuzuia shughuli zote za kisiasa za chama hicho; kutoa mgawanyo sawa wa mali zilizopo, kwa madai kuwa kinaendesha shughuli zake, bila kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano.