MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeeleza wasiwasi kuhusu kile uliodai kuwa ni matumizi ya makosa makubwa ya jinai, yakiwemo uhaini, ugaidi na uhujumu uchumi, dhidi ya Watanzania wanaoonekana kuwa na misimamo inayopingana na Serikali.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza leo 30 Julai 2026, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa, alisema mwenendo huo unazua maswali kuhusu ulinzi wa haki za binadamu na utawala wa sheria nchini.
Wakili Olengurumwa amesema mashitaka ya makosa makubwa yanapaswa kutumiwa kwa kuzingatia sheria, ushahidi na haki, na si kwa namna inayoweza kuonekana kuzuia wananchi kutoa maoni yao au kushiriki katika masuala ya umma.
THRDC imetoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha mifumo ya haki inafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, sheria za nchi na viwango vya haki za binadamu ili kulinda haki za msingi za wananchi na kuimarisha imani ya umma katika mfumo wa utoaji haki.
Kauli hiyo imetolewa wakati kukiwa na mjadala unaoendelea kuhusu matumizi ya sheria za makosa makubwa ya jinai nchini na athari zake kwa haki za kiraia na kisiasa.