MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeeleza kushtushwa na mabadiliko ya ghafla ya tuhuma zinazomkabili Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage, ukibainisha kuwa maelezo yaliyotolewa na Jeshi la Polisi yanakinzana na yale yaliyowasilishwa mahakamani.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
​Taarifa hiyo imetolewa leo 30 Julai 2026, na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, kufuatia hatua ya mhadhiri huyo kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kushtakiwa kwenye Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 16278 ya 2026 kwa tuhuma za kigaidi.
​THRDC imebainisha kuwa, wakati Mhadhiri Kaijage akishikiliwa na polisi kinyume cha sheria kwa siku 12, sababu za awali zilizoelezwa mbele ya Mahakama Kuu zilihusu madai ya kuhamasisha maandamano. Hata hivyo, mara baada ya Mahakama Kuu kuamuru aachiwe kwa dhamana 21 Julai 2026, polisi walibadili maelezo hayo na kumfungulia mashtaka mapya ya kutishia kuchoma majengo ya umma na makazi ya polisi.
​Wakili Olengurumwa amesisitiza kuwa mabadiliko hayo ya ghafla ya mashtaka mara baada ya amri ya mahakama ya kutoa dhamana yanaibua maswali mazito kuhusu uthabiti wa tuhuma hizo, uwazi wa upelelezi, na dhamira ya kulinda haki za kikatiba.
​Kutokana na utata huo unaotishia uhuru wa kitaaluma na utawala wa sheria nchini, THRDC imetoa wito kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuifuta mara moja kesi hiyo kwa kuwa haina maslahi kwa umma.