WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Tanzania haina tatizo la ugaidi, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba cheo si kinga ya mtu kukamatwa endapo atabainika kuvunja sheria.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam ….(endelea).
Akizungumza leo visiwani Zanzibar, Katambi alifafanua kuhusu taarifa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na Sheria ya Kuzuia Ugaidi.
Alisema sheria hiyo inakataza mtu yeyote kutishia, kupanga, kuratibu au kutekeleza vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi, kuvunja sheria au kuathiri haki za wengine.
Alisema Serikali, kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, itaendelea kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa, huku akiwataka wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo kwa amani na utulivu.
Katambi pia alisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuheshimu misingi ya utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa mahakama katika kushughulikia masuala yote ya kisheria.
Aidha, alieleza kuwa mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma za jinai atafikishwa kwenye vyombo husika vya uchunguzi na baadaye mahakamani, ambapo ushahidi na vielelezo vinavyohusiana na tuhuma zake vitawasilishwa kwa mujibu wa sheria.
Pamoja na kusisitiza kuwa Tanzania haina matukio makubwa ya ugaidi, Katambi alisema bado kuna uwezekano wa kuwepo viashiria vya vitendo vya kigaidi.
Alifafanua kuwa ugaidi hauhusishi mashambulizi pekee, bali pia vitendo vya kutishia, kupanga njama, kuandaa vifaa au shughuli zinazoweza kusababisha madhara makubwa na kuvuruga shughuli za kijamii na kiuchumi.